Maandalizi ya kaukau (Crispy) za vitunguu maji

Na Mlelwa Kiwale
26 Aug 2024
Tumezoea kuona aina mbalimbali za mapishi yanayohitaji vitunguu maji ambavyo ni miongoni mwa viungo muhimu jikoni. Kuanzia maandalizi ya kachumbari, pilau, mboga na aina nyingine za mapishi kitunguu maji kimekuwa kiungo muhimu ambacho huongeza ladha na kuwavutia walaji. Mbali na mapishi ya vyakula hivyo wapo wanaotumia kitunguu maji katika masuala ya urembo wa ngozi na […]
article
  • Kaukau za vitunguu maji ni miongoni mwa vitafunwa rahisi unavyoweza kuandaa nyumbani.
  • Kitafunwa hiki husindikizwa na aina yoyote ya kinywaji utakachopendelea.

Tumezoea kuona aina mbalimbali za mapishi yanayohitaji vitunguu maji ambavyo ni miongoni mwa viungo muhimu jikoni.

Kuanzia maandalizi ya kachumbari, pilau, mboga na aina nyingine za mapishi kitunguu maji kimekuwa kiungo muhimu ambacho huongeza ladha na kuwavutia walaji.

Mbali na mapishi ya vyakula hivyo wapo wanaotumia kitunguu maji katika masuala ya urembo wa ngozi na nywele wakidai kuziongezea virutubisho na mvuto.

Hata hivyo, ubunifu wa kutumia kiungo hicho bado unaendelea na hivi sasa unaweza kutumia kitunguu maji kutengeneza kaukau au maarufu kama ‘cripsy’ ambazo zinaweza kutumia kama kitafunwa au kiburudisho kinachoweza kusindikizwa na kinywaji baridi.

Tukiachana na ‘cripsy’ za viazi mviringo, viazi vitamu, ndizi na mihogo, Jikopoint imekuletea maandalizi rahisi ya kaukau hizo zinazotumia muda mchache kuandaa.

Tupike pamoja

Haya sasa mdau wa jikopoint, tuanze mapishi yetu kwa kuandaa vitunguu ambavyo ndiyo mahitaji ya msingi katika pishi tunaloliandaa.

Hakikisha umechagua vitunguu vikubwa ambavyo havijakaa muda mrefu sokoni au kupigwa na jua kwa muda mrefu ili kaukau zako zisiwe na ladha kali isiyovutia.

Tuendelee na mapishi kwa kumenya na kuosha vitunguu kisha kuvikatakata kwa saizi ya duara na uviweke kwenye chombo kisafi vikauke maji.

Vitunguu vikikauka maji viweke kando, chukua bakuli safi na uanze kuweka ngano kiasi kulingana na wingi wa vitunguu kisha utakuwa unatumia ngano hiyo kupakazia vitunguu vyako.

Utachukua bakuli lingine na kuanza kuweka ngano, paprika, maji, chumvi  na pilipili manga kiasi kama utapendelea ili utengeneze mchanganyiko mzito kama ule wa kutengenezea chapati za maji au keki, utavichanganya kwa pamoja hadi viungo vikolee vizuri.

Koroga mpaka vitunguu vichanganyike vizuri na ngano kisha uanze kutoa duara la kitunguu kimoja kimoja na kuupakaza unga wa ngano ili kuzifanya viwe vikavu zaidi.

Wakati unaendelea na hatua hiyo washa jiko, bandika kikaangio na uanze kuweka vitunguu vilivyopitishwa katika unga wa ngano mkavu na uache jikoni mpaka viive.

Hakikisha moto ni wa wastani ili visingue na utavipika mpaka vibadiike kuwa rangi ya kahawia hapo vitakuwa tayari kwa ajili ya kula vikisindikizwa na aina yoyote ya kinywaji utakachopendelea.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa