Kiburu: Ni ndizi na maharage pamoja

Na Lucy Samson
31 Aug 2022
Ni chakula cha asili ambacho hupikwa kwenye chungu kwa kuchanganya maharage, ndizi na viungo kama nyanya na kitunguu.
article
  • Ni chakula maarufu kwa kabila la Wachaga.
  • Ndizi na maharage vinachanganywa na kusongwa pamoja.

Kama umetembelea mji wa Kilimanjaro na hujapata bahati ya kula “kiburu” basi utakuwa hujatendea haki safari yako mkoani humo.

Kiburu ni moja kati ya chakula maarufu cha jamii ya Wachaga wanaopatikana mkoani Kilimanjaro. Ukikutana nao hawataacha kukuhadithia utamu wa vyakula vyao vya asili ikiwemo chakula hiki cha kiburu.

Chakula hiki ni mchanganyiko wa ndizi na maharage ambavyo husongwa vizuri ili kutengeneza mchanganyiko mzito ambao ndiyo kiburu chenyewe.

Kiasili chakula hiki hupikwa kwenye chungu, ila kimjini mjini unaweza kupika kwenye sufuria tu na msosi wako ukawa mtamu.

Mahitaji

  • Ndizi mshale 
  • Maharage
  • Kitunguu
  • Chumvi 
  • Magadi na mafuta ya kupikia

Maandalizi

Anza kwa kumenya ndizi kutokana na wingi wa watu watakao kula pishi lako. Mimi nitatumia ndizi za Sh2,000 zinanitosha kwa mlo wa mchana na jioni.

Ukishamenya ndizi zikate vipande vidogo vidogo na uzioshe kwa maji safi kisha uzitoe maji na uziweke pembeni.

Chambua maharage, yaoshe na uyabandike jikoni mpaka yaive.

Yakikaribia kuiva ongeza ndizi, kitunguu, mafuta, chumvi, magadi kiasi  na maji kisha ufunike mpaka ndizi na maharage yaive vizuri.

Zikishaiva ziepue na usubiri zipoe kidogo ili uweze kusonga na kutengeneza mchanganyiko mzito.

Endelea kusonga huku ukiongeza maji ya moto kidogo kidogo mpaka uridhike na ulaini wa mchanganyiko wako.

Ukimaliza kusonga rudisha tena jikoni uchemke kidogo, kama uliweka maji mengi acha jikoni mpaka uridhike na uzito wa kiburu chako.

Ukihakikisha chumvi imekolea na pishi lako limechemka vizuri hapo kiburu chako kitakuwa tayari kuliwa. Unasubiri nini? Kaa sogea mezani na uwapendao kufurahia chakula.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa