‘Kishumba’: Ndizi, maharage vinaposongwa kama ugali

Na Edda Mturi
9 Sept 2022
Chakula hiki ni mchanganyiko wa ndizi na maharage ambazo huchanganywa pamoja na husongwa na huwa mzito kama ugali.
article
  • Chakula maarufu cha kabila la Wapare.
  • Kinapikwa kwa ndizi na maharage vikisongwa kama ugali.

Kishumba ni moja ya chakula maarufu cha kabila la Wapare wanaopatikana mkoani Kilimanjaro ambacho huliwa mchana na hata asubuhi.

Chakula hiki ni mchanganyiko wa ndizi na maharage ambazo huchanganywa pamoja na husongwa na huwa mzito kama ugali.

Kiasili chakula hiki hupikwa kwenye chungu na jiko la kuni. Kwa sasa unaweza kupikia kwenye sufuria lakini ladha na utamu wake ni ule ule.

Unahitaji kuwa na ndizi, maharage, chumvi, magadi, kitunguu na mafuta ya kupikia.

Maandalizi

Menya ndizi kutokana na idadi ya watu watakaokula pishi lako, kisha zikate vipande vidogo vidogo na uzioshe kwa maji safi na uziweke pembeni.

Chambua maharage, yaoshe na uyabandike jikoni mpaka yaive.

Yakikaribia kuiva weka ndizi, kitunguu, mafuta kidogo, magadi na maji kisha ufunike mpaka ndizi na maharage yaive vizuri.

Zikishaiva ziipue na usubiri zipoe kidogo ili uweze kusonga  mpaka ziwe nzito. Hapo pishi lako litakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kula asubuhi na chai hata mchana.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa