Maandalizi rahisi ya wali na rosti ya maini

Na Lucy Samson
25 Apr 2023
Fikiria upate wali wako uliopikwa vizuri na kusindikizwa na rosti ya maini iliyokolea viungo.
article
  • Ni moja ya chakula kitamu unachoweza kujipikia nyumbani.
  • Maandalizi yake ni rahisi unaweza kupika kwa muda mchache.

Haijalishi uwe wali wa nazi au wali wa kawaida, utamu wa msosi huu haupimiki.

Fikiria upate wali wako uliopikwa vizuri na kusindikizwa na rosti ya maini iliyokolea viungo.

Haya yote unaweza kuyaandaa nyumbani kwako kwa maandalizi rahisi na mahitaji machache na ukafurahia pamoja na familia.

Tuingie jikoni

Leo tutapika wali wetu kwenye jiko la umeme maalum (rice cooker) ambalo hupika kwa muda mchache.

Hatua ya kwanza kabisa chambua mchele, osha kisha andaa ‘rice cooker’ kwa ajili ya kupika wali.

Pima kiasi cha maji, weka chumvi kiasi mafuta na ukoroge chumvi ichanganyike, baada ya hapo weka mchele funika na uwashe jiko lako ili wali uanze kujipika.

Wakati wali unaiva andaa maini, yaoshe na uyakatekate saizi uipendayo.

Menya nyanya na uzisage, kata kitunguu, karoti, hoho na tangawizi kiasi utakazozitumia kwenye kuunga rosti lako.

Tuanze kukaangiza

Kwenye hatua hii tuanze na kuweka mafuta jikoni, yakipata moto tuongeze kitunguu ambavyo unatakiwa kukoroga mpaka viwe na rangi ya kahawia.

Baada ya hapo ongeza tangawizi, hoho na karoti na ukoroge kwa dakika moja kisha umalizie na nyanya ulizosaga au nyanya za pakti kisha uache viive.

Vikiiva weka maini na uache yaive kwa dakika 10 au zaidi kutokana na wingi wa maini yako.

Kama uliyachemsha au kukaanga maini huna haja ya kuacha jikoni kwa muda mrefu.

Koroga mboga yako ongeza chumvi, maji ya ndimu na pilipili kisha ikichemka, mboga yako itakuwa tayari.

Tusishau tumeweka wali kwenye ‘rice cooker’ hivyo baada ya muda angalia wali wako kama umeiva kisha epua na uandae kwa ajili ya kuliwa.

Ukiwa na ‘rice cooker’ huna haja ya kuhofu kuhusu wali kuungua, mara nyingi majiko haya ya kisasa hujizima yenyewe chakula kikiiva.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa