Tangawizi na kitunguu swaumu ni miongoni mwa viungo muhimu katika mapishi ya kila siku, uwepo wake katika mboga huongeza ladha na harufu nzuri inayovutia.
Licha ya umuhimu wake katika mboga, kuandaa viungo hivi kila siku huchosha hususan kama unapika chakula cha watu wengi kinachohitaji viungo hivyo.
Habari njema ni kwamba unaweza kutengeneza mchanganyiko wa viungo hivyo ukavihifadhi kwa muda mrefu wa zaidi ya wiki tatu na kuokoa gharama pamoja na muda wa kuviandaa kila siku.
Mchanyiko huu pia unaweza kuwa biashara itakayokuingiza kipato kuanzia 2500 mpaka Sh5000 kutengemea na vifungashio utakavyotumia.
Karibu jikoni tujifunze na tuandae kwa pamoja mchanganyiko wa tangawizi na kitunguu swaumu.
Jinsi ya kutengeneza
Osha tangawizi, menya na uzikate vipande vidogo vidogo weka kwenye bakuli kisha hamia kwenye kumenya vitunguu swaumu, ongeza chumvi kiasi tayari kwa ajili ya kusaga.
Katika hatua hii unaweza kusaga kwa kutumia blenda ya umeme, kisagio cha mkono au kutwanga na kinu,cha muhimu viungo vyako vilainike vizuri.
Kama unatumia blenda ya umeme au kinu ongeza maji, mafuta na ‘vinegar’ wakati unasaga aukutwanga ili kusaidia viungo kulainika kwa urahisi na kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika.
Unaweza kuongeza viungo zaidi kama kotmiri na vinginevyo katika mchanganyiko wako ili kuonngeza ladha na harufu nzuri.
Viungo vikisagika vizuri mchanganyiko wako utakuwa tayari kwa kutumiwa.
Mambo ya kuzingatia
Ili mchanganyiko huu uweze kudumu kwa muda mrefu ni lazima uhifadhi kwenye friji au kama utatumia njia ya kawaida basi tumia chombo chenye mfuniko usiopitisha hewa.
Hakikisha unatumia mafuta, chumvi na ‘Vinegar’ ya kutosha ikiwa hautumii friji kuhifadhi ili viungo vyako viweze kudumu kwa muda mrefu zaidi.