Maandalizi ya mchemsho wa viazi na samaki

Na Lucy Samson
20 Mar 2023
Mchemsho huu unaweza kuwa mbadala wa vyakula vya haraka (fast food) au vyenye mafuta mengi vinavyoongeza uzito.
article
  • Ni moja kati ya chakula maarufu kinacholiwa wakati wa asubuhi.
  • Unafaa kutumiwa na watu wote hususani wagonjwa na waliopo kwenye diet.
  • Ni rahisi kuandaa nyumbani.

Mchemsho wa viazi na samaki  ni moja ya kifungua kinywa maarufu kwa baadhi ya sehemu nchini Tanzania hususani majiji makubwa kama Dar es Salaam.

Umaarufu wa msosi huu unatokana na urahisi wa upatikanaji wake kuanzia kwenye migahawa ya mama ntilie mpaka kwenye hoteli kubwa.

Uwepo wa samaki na mbogamboga kwenye pishi hili unalifanya kuwa moja kati ya mapishi yenye virutubisho yanayofaa kuliwa na watu wote.

Kwa wale waliopo kwenye utaratibu maalum wa kujipimia chakula (diet) hapa ndio penyewe. Mchemsho huu unaweza kuwa mbadala wa vyakula vya haraka (fast food) au vyenye mafuta mengi vinavyoongeza uzito.

Mpaka hapa natumaini una shauku ya kujifunza, usijali JikoPoint (www.nukta.co.tz)  ipo kwa ajili yako, sogea jikoni 

Unasubiri nini tuingie jikoni

Tuanze maandalizi wetu kwa kuandaa samaki. Unaweza kutumia samaki wa maji baridi kama sato, sangara au hata wa baharini pishi litanoga.

Osha samaki wako, mparue magamba kama anayo, mtoe utumbo wa ndan na  uhakikishe ni msafi na muweke kwenye chombo kisafi kisha mfunike.

Andaa viungo na mbogamboga upendazo, unaweza kuandaa karoti, hoho, kitunguu maji, ukipenda unaweza kuongeza bilinganya, bamia  au nyanya chungu.

Menya viazi, osha na uvikate kate, usisahau kusaga tangawizi, kitunguu swaumu na kuandaa ndimu itakayokusaidia kukata shombo ya samaki na kuongeza ladha.

Mboga mboga kwenye pishi la mchemsho wa viazi na samaki huongeza virutubisho mwilini na kuufanya mwili kuwa na afya.Picha|Malkia kitchen/YouTube.

Baada ya maandalizi yote hayo tuhamie jikoni sasa, washa jiko lako la gesi au la umeme bandika sufuria yako na uanze kwa kuweka samaki chini viungo kisha malizia na viazi kwa juu na maji yanayotosha kuivisha.

Tunafanya hivi ili kuruhusu samaki aive vizuri na kupuguza uwezekano wa viazi kurojeka.

Funika pishi lako na uache liive kwa dakika 20 au zaidi kisha uongeze hoho na karoti, pilipili, ndimu na mbogamboga ambazo tuliacha mwanzoni.

Baada ya dakika tano hivi utaanza kusikia harufu nzuri ya kuvutia itakayokuthibitishia mchemsho wako wa viazi na samaki upo tayari kwa kuliwa.

Unaweza kuongeza chapati ama ukala mchemsho wako wenyewe tu na ukafurahia.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa