Majani ya mlonge yanavyoweza kutumika kama chakula

Na Edda Mturi
29 Aug 2022
Unaweza kuyapika kwa kitunguu na nyanya. Ni mboga nzuri unayoweza kula na wali au ugali.
article
  • Unaweza kuyapika kwa kitunguu na nyanya.
  • Ni mboga nzuri unayoweza kula na wali au ugali.

Mlonge ni mti maarufu kwa sasa duniani. Unatumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo tiba kwa sababu karibu kila sehemu ya mti huo ina matumizi yake.

Kutoka maua, majani, mbegu, magome na matunda kote huko utapata faida endapo utaamua kujifunza matumizi yake. Mfano, mbegu za mti huu ni dawa ya magonjwa sugu kama vile vidonda vya tumbo, magonjwa ya ngozi na kisukari. Maua na majani yake yanaweza kupikwa kama mlenda au mboga.

Leo tunaangazia namna unavyoweza kupika majani ya mlonge kama mboga.

Mahitaji

Utakachohitaji ni mafuta, chumvi, vitunguu maji kutokana na wingi wa majani yako. Kama ni machache kitunguu kimoja tu kinatosha, bamia na nyanya mbili. Pia unaweza kuongeza  nazi au karanga.

Maandalizi

Chambua majani ya mlonge, yaoshe kwa maji safi na salama kisha menya kitunguu na nyanya kama utatumia. Kumbuka nyanya siyo lazima kutumia.

Washa jiko lako la gesi au umeme na uchemshe majani yako. Yakiiva weka pembeni, chukua sufuria nyingine weka mafuta kiasi kaanga kitunguu mpaka kiwe na rangi ya kahawia. Baada ya kitunguu kuiva weka majani na chumvi itakayotosha.

Funika nasubiri iive. Hapa unaweza kuongeza chumvi kama haijakolea. 

Pishi letu likishaiva litakuwa tayari kwa kuliwa. Mboga hii inaweza kuliwa kwa ugali au wali ikiwa na mboga nyingine pembeni.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa