Makande ya nyama: Mahitaji, jinsi ya kupika

Na Lucy Samson
8 Feb 2023
Makande ya nyama, ni moja kati mapishi matamu sana, unayoweza kula mchana au usiku, lakini si wengi wanafahamu jinsi ya kupika pishi hilo.
article
  • Ni namna nyingine ya kuongeza ubunifu kwenye mapishi
  • Chakula hiki kinafaa sana kwa familia yenye watu wengi
  • Utakachohitaji ni nyama, mahindi yaliyokobolewa, maharahe na viungo.

Nilipokuwa mdogo nilipenda sana makande ya maharage kiasi kwamba nilimsumbua mama ayapike kila wiki.

Hata nilipoanza shule ya bweni sikuona shida kabisa kula chakula hicho ambacho kilichukiwa na baadhi ya  wanafunzi kutokana na kutokupikwa vizuri.

Mapenzi yangu na chakula hicho yaliendelea hadi pale nilipokutana na makande ya nyama yaliyopikwa na mmoja wa wenyeji wangu mkoani Kilimanjaro.

Makande ya nyama? nilihoji kwa kushangaa  kutokana na ukweli kwamba sikuwahi kuonja chakula hicho.

Basi bwana msosi ukaletwa mezani, nikaonja kijiko cha kwanza, cha pili nilipofika kijiko cha tatu nikashindwa kuvumilia ikabidi nikisifie, chakula kilikuwa kitamu sana hata nikaomba kuongezewa.

Baada ya kula nikaomba kufundishwa namna ninavyoweza kupika chakula hicho chenye ladha ya pekee.

Leo nimeona nikuletee ujuzi huu niliofundishwa ili na wewe uweze kufurahia chakula hiki na familia yako.

Maandalizi

Hatua ya kwanza kabisa kwenye upishi huu ni kuchambua mahindi, maharage au njugu kwa wale wasiotumia maharage na kuyaosha vizuri.

Baada ya kuosha washa jiko na uanze kwa kubandika maharage au njugu na  baada ya dakika 30 uongeza mahindi.

Wakati unasubiri mahindi yaive katakata nyama, osha na uongeza kitunguu swaumu, tangawizi na chumvi kisha uchemshe mpaka iive.

Ili kupika makande ya nyama yenye ladha nzuri ni vyema kuzingatia uchaguzi mzuri wa mahindi, maharage au njugu.Picha|Nukta Habari.

Tuunge makande yetu sasa

Makande na nyama vikiiva hatua inayofuata ni kuyaunga kwa pamoja na kutengeneza makande ya nyama.

Hapa utaanza kwa kumenya nyanya, vitunguu, karoti na hoho pamoja na kuandaa tui la nazi tutakalolitumia kwenye chakula chetu.

Kwenye sufuria safi weka mafuta kiasi kaanga kitunguu mpaka kiive, kisha ongeza nyanya na ufunike ziive vizuri.

Baada ya nyanya kuiva ongeza nyama koroga na ufunike kwa dakika tano ichanganyike na nyanya.

Dakika tano zikiisha funua, koroga tena na uongeze makande, chumvi, karoti, hoho na tui jepesi  na uache ichemke kwa dakika tano au zaidi.

Pishi lako likichemka ongeza tui la pili zito. Acha ichemke kwa dakika 5 au zaidi kutegemea na wingi wa tui uliloongeza.

Baada ya kujiridhisha na kiwango cha mchuzi unachotaka msosi wako utakuwa tayari kwa kula. 

Unasubiri nini? waite marafiki na ndugu wafurahie msosi huu wenye faida nyingi mwilini ikiwemo kukupa nguvu na muonekano mzuri.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa