Mambo muhimu ya kufahamu kuhusu chakula cha “ngararimo”

Na Lucy Samson
30 Aug 2022
Ni chakula cha asili cha kabila la Wachaga ambacho hupikwa kwa mahindi yasiyokobolewa pamoja na maharage.
article
  • Chakula hiki huliwa na watu wa rika zote
  • Mahitaji yake ni pamoja na mahindi, maharage na mafuta ya kupikia.
  • Mengine ni magadi, nyanya na hoho.

Ngararimo ni chakula cha asili cha kabila la Wachaga wanaopatikana zaidi mkoani Kilimanjaro. Chakula hiki hupikwa kwa mahindi yasiyokobolewa pamoja na maharage.

Chakula hiki huliwa na watu wa rika zote, kasoro watoto wadogo ambao hawajaota meno na wazee wasioweza kutafuna.

Kiasili chakula hiki hupikwa kwenye chungu, ila unaweza pia kukipika kwenye sufuria ya kawaida na bado ukafurahia msosi huu.

Mahitaji ya chakula hiki ni mahindi, magadi, maharage, nyanya, kitunguu, chumvi, mafuta, karoti na hoho.

Maandalizi

Hatua ya kwanza katika mapishi chakula hiki ni kuchambua mahindi pamoja na mharage, kuyaosha na kuyaweka kwenye bakuli mbili tofauti.

Washa jiko bandika sufuria yenye maji yakikaribia kuchemka weka mahindi na magadi vijiko 2 vya chakula na ufunike.

Ongeza maji kila yanapokaribia kuisha ili mahindi yako yasiungue.

Yakikaribia kuiva, yaipue uyamimine kwenye  sufuria nyingine kubwa na uyaache yapoe kwa ajili ya kuyaondoa maganda ya juu.

Yakishapoa anza kwa kuyaongezea maji kisha uyapekeche kwa mpekecho au uyasugue kwa mikono. 

Hatua hii inafanyika ili kuondoa maganda ya mahindi.

Kama bado unaendelea kuona maganda ya mahindi rudia tena hatua hii mpaka maganda yatoke yote.

Maganda haya huondolewa ili kuondoa sumu kuvu ambayo wataalamu wa lishe wanasema inakaa kwenye mahindi lakini pia, kuwezesha mahindi haya kuwa malaini ili yaweze kuliwa hata na wazee.

Baada ya kuyaondoa maganda yabandike pamoja na maharage ongeza magadi  na maji na uyaache  mpaka yaive vizuri. 

Wakati unasubiri yaive kaanga kitunguu, nyanya, karoti na hoho pembeni kwa ajili ya kuunga ngararimo zako.

Mahindi na maharage yakiiva weka chumvi, kisha mimina mchanganyiko wa kitunguu na nyanya uliuokwisha kukaanga, koroga na uache mpaka zichemke.

Zikichemka hakikisha mchuzi umepungua kwa kiasi ukipendacho, kisha ngararimo zitakuwa tayari kuliwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa