Manufaa ya kula senene kama chakula

Na Mariam John
17 Jun 2022
Senene huliwa kama kitoweo na huweza kulia kwa mlo wa mchana au usiku hasa ugali wa unga wa mahindi au mhogo.
article
  • Wadudu hao wana protini na madini ya chuma.
  • Hupatikana zaidi katika Mkoa wa Kagera.
  • Maandalizi yake ni rahisi na unaweza kuwala kwa ugali, wali au ndizi.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), kuna wadudu aina 1,900 ambao wanaweza kuliwa duniani. Wengi wa wanaoliwa ni mende, viwavi, nyuki, nyigu, nzige, kumbikumbi, nge, vipepeo na kerengende.  

Kwa Tanzania, senene ni miongoni wadudu wanaoliwa na watu wengi. 

Senene ni wadudu jamii ya panzi. Wadudu hawa ni chakula cha asili cha baadhi ya makabila nchini Tanzania wakiwemo Wahaya wanaoishi mkoani Kagera.

Wenyeji wa mkoa huo wanasema senene wamekuwepo enzi na enzi na wamekuwa wakikitumia kitoweo hicho kama chakula.

Senene hutumiwa kama kitoweo na huweza kulia kwa mlo wa mchana au usiku hasa ugali wa unga wa mahindi au mhogo. Wengine hutumia kitoweo hiki na ndizi za kuchoma au kutafunia na kikombe cha kahawa au chai majira ya jioni na asubuhi.

Pamoja na kutumiwa kama kitoweo, senene ni chanzo cha ajira na kwa vijana wanakopatikana wadudu hao.

Oscar Mihayo ni mzaliwa wa Mkoa wa Kagera kwa sasa anaishi Kirumba jijini Mwanza, anasema zamani kitoweo hicho kilitumika kwa chakula pekee lakini kutokana na wenyeji wa mkoa huo kusambaa katika maeneo tofauti nchini ni fursa ya kujipatia kipato.

Anasema hivi sasa katika maeneo mbalimbali jijini Mwanza, Geita, na Dar es Salaam vijana huuza kitoweo hicho lakini pia kwenye maeneo ya maduka makubwa (supermarket) wadudu hao unaweza kuwapata.

Senene wanatajwa kuwa na faida nyingi kwa mwili wa binadamu ikiwemo kuupatia protini na madini ya chuma.

Namna ya kuandaa senene

Baada ya kuvunwa, senene huchambuliwa kwa kuwaondoa mabawa na miguu kisha husafishwa kwa maji safi na kuwekwa jikoni.

Baada ya maji kukauka mpishi ataendelea kukaaga hadi wakauke vizuri na kuweka chumvi. Mbali na kukaanga kwa kutumia maji pekee pia kitoweo hicho hukaangwa  kwa kutumia mafuta.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa