Najua unazifahamu sifa za jiji la Tanga, husuan ile ya uwepo wa nazi nyingi zinazotumika kuandaa mapishi mbalimbali.
Kutokana na kuenea kwa sifa hizo nikadhamiria kwenda kumtembelea rafiki yangu anayeishi Pangani Jijini Tanga, kichwani nikawaza kkumuandalia chai ya nazi ambayo si maarufu sana katika maeneo haya.
Lengo la kuvutiwa na aina hiyo ya kifungua kinywa ni kuwadhihirishia wakazi wa jiji hilo kuwa hata watu wa mikoa mingine tupo vizuri kwenye mapishi.
Baada ya kuandaa chai hiyo, rafiki yangu aliipenda sana na ‘kunimwagia maua yangu’ nikasema acha nije niwafundishe wasomaji wa jiko point wapate kuongeza ujuzi na maujanja jikoni.
Mahitaji
Kwanza ukitaka kupika chai hii utahitaji tui la nazi zito kikombe 1 na robo, hapa unaweza kutumia nazi freshi au ya pakiti inayopatikana kirahisi madukani.
Utahitaji maji safi kikombe kimoja na nusu ili kuongeza wingi wa chai yako, majani ya chai kijiko kimoja cha chai, sukari kiasi kulingana mahitaji yako, iriki, mdalasini, majani ya oregano, mints (nanaa) pamoja na karafuu kama unapendelea.
Karibu jikoni tuandae pamoja
Anza mapishii yako kwa kusafisha sufuria utakayopikia, washa jiko, na ubandike sufuria na umimine maji pamoja na tui lanazi uliloliandaa.
Hatua inayofuata ni kuweka viungo vyote vinavyohitajika katika pishi hili. Hakikisha umevitwanga na kuchekecha vizuri kisha uache ichemke.
Kama ilivyo kwa mapishi mengine yanayotumia nazi, ni mwiko kufunika chai yako kabla haijachemka ili kuzuia tui kukatika.
Mchanganyiko ukianza kuchemka punguza moto kiasi kisha acha ichemke taratibu ili iingie viungo kwa muda wa dakika sita.
Ongeza tena tena moto kama awali na acha ichemkie kwa muda wa dakika 10 kisha epua,chuja na itakuwa tayari kwa kunywa.
Chai hii ni tamu sana na unaweza kuinywa kwa vitafunwa mbalimbali kama vile skonzi, mandazi ya kuoka, chapati za amira, na aina nyingine nyingi.