Kababu ni miongoni mwa vitafunwa maarufu ambavyo hupikwa kwa aina yake vikivutia walaji kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Kitafunwa hiki huweza kupikwa kwa kutumia nafaka na vitowe mbalimbali zikipewa majina tofauti mfano, kababu za kuku ambazo hupikwa kwa nyama ya kuku, kababu za nyama ya ngombe na samaki ambazo zote hupikwa kulinga na matakwa ya mpishi au mlaji.
Katika aina hizo za kababu, Jikopoint tumekusogezea mapishi ya kababu zilizopewa jina la jicho la mke mweza zinazopikwa kwa nyama ya ngombe na mayai.
Pishi hili linafaa sana kutumiwa kama sehemu ya kifungua kinywa, kwa waliopo kwenye mfungo wa ramadhani au kwaresma wanaweza kulitumia kama sehemu ya ftari.
Mahitaji
Namna ya kupika hatua kwa hatua
Hatua ya kwanza ni kununua mahitaji yote ya msingi yanayohitajika katika upishi huu ili kuepuka usumbufu wa kutafuta mahitaji iwapo utachelewa kufanya manunuzi mapema.
Baada ya hapo, anza na maandalizi ya nyama ya kusaga ambayo baada ya kuiosha utaibandika jikoni ukiongeza mafuta ya kula kiasi, ndimu au limao na unga wa ngano kisha utaipika kwa dakika nne mpaka tano kwa moto mdogo mpaka pale itakapobadilika rangi na kuiva.
Weka nyama katika bakuli kubwa na uiache ipoe kisha uendelee na mapishi kwa kuchemsha mayai uliyopanga kutumia huku ukibakisha yai moja ambalo utalitumia katika hatua nyingine za mapishi.
Mayai yakiiva yaache yapoe, kisha yamenye na uyakate kati kati ili kupata vipande viwili na utenganishe kiini cha yai ambacho utakichanganya na nyama ya kusaga.
Baada ya hapo changanya katika bakuli lenye nyama na viini anza kuchanganya nyama na viini mpaka vichanganyike vyote vikisha changanyika chukuwa mayai yale meupe uliyotoa viini pakia nyama uliyochanganya na viini kwa ndani kutengeneze umbo la yai huku ukijaza nyama ndani ya hayo mayai meupe yote mpaka yaishe.
Kwenye mchanganyiko ndani ya bakuli vunjia yai moja bichi lililobaki weka na unga wa ngano kidogo kisha changanya mpaka madonge ya unga yalowe halafu bandika karai la mafuta jikoni hakikisha moto unatumia wa wastani usije kuunguza.
Mafuta yakishapata moto kiasi chukuwa yai moja moja katika yale uliyoyajaza nyama ndani chovya katika yai ulilochanganya na unga hakikisha umelichovya sehemu zote kisha dumbukiza katika karai la mafuta kaanga pande zote mbili.
Rudia hatua hiyo kwa mayai yote yaliyobaki, ukimaliza kukaanga pishi la jiko la mke mweza litakuwa tayari kuliwa na unaweza kula kwa kutumia chatney yoyote.
Kumbuka tu sio lazima kutumia nyama ng’ombe, unaweza kutumia nyama aina nyingine kama nyama ya kuku, ya mbuzi, ya bata au unaweza kutumia samaki ukitaka ni wewe tu.