Maujanja ya kupika mchele usio na kiini

Na Rodgers George
28 Oct 2021
Unaweza kuangazia matumiz ya foil paper kwenye kupika wali usiokuwa na kiini.
article

  • Ni kwakutumia foil paper kunasa mvuke.
  • Itasaidia kuondoa kiini kwenye wali uliopika.
  • Ni mbadala wa majani ya mgomba yaliyokuwa yakitumika zamani.

Dar es Salaam. Kama ndiyo unajifunza kupika wali, huenda ukapata ukakasi wa mbinu gani utumie ili kupata chakula kilichokamilika.

Upishi wa wali una mbinu mbalimbali ambazo kila mpishi amezoea.

Mpishi huyu anaweza kupika kwa kutumia maji ya baridi na huyu akatumia maji ya moto. Huyu anaweza kukufundisha lile na huyu akakufundisha hili.

Hata hivyo, utofauti huo wote ni nadharia tu na jinsi mtu alivyo na amani katika upishi wake. Wakati wengine wakitumia mkaa au kuni kupika wali; jiko la gesi au umeme linaweza kuwa njia salama na rahisi kupika chakula hicho pendwa.

Leo nakufundisha njia ya kupika wali kwa kutumia foil paper (karatasi ya aluminiamu) huku ukitumia kiasi kidogo cha nishati yako ya gesi au umeme.

Hauwezi kufurahia kula wali ambao haujaiva vizuri. Picha| The Kitchen Community.

Foil paper na mapishi ya ubwabwa

Kwanza, kama ulikuwa unatumia maji ya baridi kupika mchele, ni vyema ukaacha sasa. Hiyo inafanya mchele uchukue muda mwingi zaidi kuiva kwani nguvu nyingi ya nishati itatumika kuchemsha maji ya baridi baada ya kuanza mapishi yako.

Inashauriwa uchemshe maji kabla na kuyaweka kwenye chombo iwe jagi au sufuria.

Baada ya kuwa umeshachambua mchele wako, na umeshaosha, hatua ya kwanza ya kupika wali ni kuweka sufuria lako kwenye jiko na kisha kuwasha moto wako. 

Kisha weka mafuta kiasi unachopendelea na yakichemka, weka mchele wako ndani ya sufuria hilo. Kaanga kwa sekunde chache kisha weka chumvi na ukichanganya vyema, weka maji uliyokuwa umeyaandaa (ya moto).

Chukua foil paper na funikia pishi lako na juu ya foil paper, weka mfuniko wako.

Hatua hiyo itaepusha mvuke kutoka wakati unapika na hivyo wali kuiva haraka na kuondoa kiini (ugumu ambao hubaki kwenye wali usipoiva vizuri). Wakati huo huo hakikisha moto wa jiko lako uko kawaida.

Kufunika wali na foil paper itasaidia kunasa mvuke ili wali uive vizuri. Picha| Pinterest.

Acha pishi lako liive na maji yaliyokuwa yamezidi kimo cha wali yapungue kiasi cha maji kutokuonekana kabisa. Kupungua maji inaweza kukadiliwa kuwa ndani ya dakika tano. 

Bada ya muda (makadilio ya ndani ya dakika zisizozidi tano) funua mfuniko na maji yaliyokuwa yameuzidi mchele yatakuwa yamepungua kabisa.

Unaweza kuongeza mbwembwe kwenye wali wako kwa kuweka vipande vidogo vidogo vya karoti, zabibu kavu na hata korosho. 

Funika tena pishi lako na lipatie dakika zingine tano huku moto ukiwa kwenye asilimia kama 20 hivi.

Baada ya hapo, wali wako utakuwa umeiva na utakuwa umepika wali usio na kiini.

Njia ya foil paper ni kama ile iliyotumika zamani a wengine wanayotumia kwa sasa ambapo wengine walikuwa wakitumia majani ya mgomba na hata mifuko ya plastiki.

Unangoja nini mzee baba? Ingia jikoni na uumize majirani kwa wali wa chapu chapu.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa