Dar es Salaam. Kwa kawaida mabachela wengi huwa tunakimbia kuandaa vitafunwa, tukihisi kuwa vitatumalizia muda na ni vigumu kutengeneza.
Njia rahisi huwa ni kununua tu vilivyoandaliwa kutoka kwa mikahawa au mamantilie wa jirani.
La hasha, kuna aina nyingi ya vitafunwa rahisi ambavyo unaweza kujiandalia mwenyewe nyumbani si unakumbuka maujanja niliyokupa kuhusu chapati za maji?
Basi na leo nakupa maujanja rahisi kabisa.‘Egg toast’ wataalam wa mapishi wanaita ivo, lakini kwa lugha rahisi ni mkate na mayai.
Pishi hili ni rahisi na linatumia dakika chache sana kukamilika, na zaidi halitatoboa mfuko wako kwani unahitaji Sh2,000 tu kwa ajili ya mahitaji.
Mahitaji muhimu
Unachohitaji ni mkate mdogo ambao umekatwa tayari (sliced bread) katika maduka ya kawaida huuzwa elfu 1, mayai matatu, chumvi robo kijiko cha chai, pamoja na mafuta ya kupikia. Unaweza kuongeza kiwango kutokana na idadi ya walaji.
Wengine hupendelea kuweka mboga mboga kama pilipili hoho, kitunguu na karoti, lakini pishi letu kwa leo hatutahitaji hivyo.
Tuingie jikoni sasa
Hatua ya kwanza, pasua mayai kwenye bakuli, kisha ongeza chumvi na ukoroge vizuri hadi mayai yatakavyo lainika.
Weka mafuta ya kupikia kijiko kimoja na nusu kwenye ‘frying pan’ au chombo chochote unachotumia kukaangia, na uweke motoni.
Hakikisha moto ni wa wastani ili usiunguze pishi lako.
Pakaza mayai kwenye kila kipande cha mkate
Hatua inayofuata, chukua kipande kimoja cha mkate na ukipakaze kwenye mayai kisha kiweke kwenye kikaangio ulichoweka mafuta.
Baada ya sekunde 30, geuza upande wa pili wa mkate na utaendelea kugeuza hadi pale mayai yatakapoiva.
Utaendelea na hatua hiyo hadi mayai yatakapoisha au kiwango cha vipande vya mkate unavyohitaji.
Unaweza kula na chai, juisi
Hadi hapo vitafunwa vitakuwa tayari, unaweza sindikizia na chai ya rangi au maziwa,lakini pia sharubati (juisi) inanogesha vitafunwa hivi.
Ukiacha urahisi na unafuu, pishi hili pia lina faida mbalimbali za kiafya, ikiwemo virutubisho vya protini bila kusahau wanga.
Maujanja ndio hayo, kazi kwako bachela mwenzangu kuanza kujiandalia mwenyewe vitafunwa nyumbani.