Kama wewe ni mpishi najua umeshawahi kukutana na changamoto au msala wa kuzidisha mafuta ya kupikia kwenye mboga au kupika supu yenye mafuta mengi.
Ni wachache tu wanaojua mbinu ya kuepuka msala huu unaoweza kufanya msosi wako ukakosa walaji.
Mbali na kukukosesha walaji, kiafya haitakiwi kuzidisha mafuta kwenye chakula kwa kuwa mafuta hayo yanaweza kuwasababishia walaji magonjwa ya moyo na presha.
Leo kwenye makala hii tutajifunza mbinu za kupunguza mafuta yaliyozidi kwenye supu au mchuzi.
Jambo la kufurahisha ni kwamba unaweza kuchagua mbinu unayoitaka kutokana na uharaka unaohitaji kuyapunguza mafuta hayo.
Fuatana nami mpaka mwisho wa makala hii ujifunze mbinu hizo.
Kugandisha supu au mchuzi kwenye jokofu
Maji na mafuta hayawezi kuchangamana, siku zote mafuta hukaa juu na maji kwa chini.
Hata kwenye supu au mchuzi wako mafuta yataelea juu hivyo ukigandisha kwa saa nne mpaka sita itakuwa rahisi kuondoa tabaka la juu la mafuta.
Ukimaliza unaweza kurudisha mboga yako au supu jikoni na kuacha ichemke tena kabla ya kutenga mezani.
Mbinu hiii nafaa sana ikiwa hauna haraka na mboga yako au supu.
Pia inaweza kupoteza ladha ya asili ya mboga yako au supu hivyo inashauriwa kuongeza viungo baada ya kuitoa kwenye jokofu.
Kupunguza mafuta kwa kutumia karatasi ya tishu
Watu wengi wamezoea karatasi za tishu zinatumika kukausha mikono au kupangusa uchafu kwenye meza za chakula.
Leo nakuongezea ujuzi kuwa unaweza kutumia tishu au kwa kimombo ‘napkins’ kupunguza mafuta yaliyozidi kwenye mchuzi.
Unachotakiwa kufanya ni kuikunja mara mbili karatasi ya tishu, kisha sika ncha za pembe tatu kwa pamoja kisha uanze kuipitisha juu ya bakuli au sufuria yenye mafuta yaliyozidi.
Tishu ina uwezo mkubwa wa kunyonya mafuta kama utaipitisha kwa juu kiasi kwamba mchuzi au maji hayataingia.
Unaweza kubadilisha tishu ukihisi imejaa. Rudia hatua hiyo mpaka utakaporidhika na kiwango cha mafuta yaliyopo.
Kupunguza mafuta kwa kutumia kijiko chenye barafu
Kwenye mbinu hii unachotakiwa kufanya ni kuweka vipande vya barafu kwenye kijiko kikubwa cha chakula na kukipitisha juu ya mchuzi au supu yako kisha kifute kwa pembeni kwenye tishu au kitambaa kisafi
Kijiko chenye barafu kinapopitishwa juu ya mafuta kinagandisha tabaka la juu la mafuta hivyo kuacha mboga yako ikiwa haina mafuta.
Kupunguza mafuta wa kutumia kijiko
Kama una haraka mbinu hii itakufaa zaidi
Unachotakiwa kufanya ni kuchota mafuta yaliyozidi kwa kutumia kijiko cha chakula.
Hata hivyo, njia hii haitapunguza mafuta kwa kiwango kikubwa kwa sababu ni rahisi sana mafuta kuchanganyika na maji wakati unachota hivyo kupunguza mchuzi badala ya mafuta.