Mbinu nne za kupunguza mafuta yaliyozidi kwenye mchuzi, supu

Na Lucy Samson
9 Nov 2022
Miongoni mwa mbinu hizo za kuondoa mafuta kwenye chakula ni matumizi ya tishu, barafu na kugandisha kwenye jokofu.
article
  • Msala huu wa kuzidisha mafuta kwenye chakula unaweza kumpata yoyote.
  • Jambo la kufurahisha ni kwamba zipo mbinu za kutatua changamoto  hii.

Kama wewe ni mpishi najua umeshawahi kukutana na changamoto au msala wa kuzidisha mafuta ya kupikia kwenye mboga au kupika supu yenye mafuta mengi.

Ni wachache tu wanaojua mbinu ya kuepuka msala huu unaoweza kufanya msosi wako ukakosa walaji.

Mbali na kukukosesha walaji, kiafya haitakiwi kuzidisha mafuta kwenye chakula kwa kuwa mafuta hayo yanaweza kuwasababishia walaji magonjwa ya moyo na presha.

Leo kwenye makala hii  tutajifunza mbinu za  kupunguza mafuta yaliyozidi kwenye supu au mchuzi.

Jambo la kufurahisha ni kwamba unaweza kuchagua mbinu unayoitaka kutokana na uharaka unaohitaji kuyapunguza mafuta hayo.

Fuatana nami mpaka mwisho wa makala hii ujifunze mbinu hizo.

Kugandisha supu au mchuzi kwenye jokofu

Maji na mafuta hayawezi kuchangamana, siku zote mafuta hukaa juu na maji kwa chini.

Hata kwenye supu au mchuzi wako mafuta yataelea juu hivyo ukigandisha kwa saa nne mpaka sita itakuwa rahisi kuondoa tabaka la juu la mafuta.

Ukimaliza unaweza kurudisha mboga yako au supu jikoni na kuacha ichemke tena kabla ya kutenga mezani.

Mbinu hiii nafaa sana ikiwa hauna haraka na mboga yako au supu.

Pia  inaweza kupoteza ladha ya asili ya mboga yako au supu hivyo inashauriwa kuongeza viungo baada ya kuitoa kwenye jokofu.

Kupunguza mafuta kwa kutumia karatasi ya tishu

Watu wengi wamezoea karatasi za tishu zinatumika kukausha mikono au kupangusa uchafu kwenye meza za chakula.

Leo nakuongezea ujuzi kuwa unaweza kutumia tishu au kwa kimombo ‘napkins’ kupunguza mafuta yaliyozidi kwenye mchuzi.

Unachotakiwa kufanya ni kuikunja mara mbili karatasi ya tishu, kisha sika ncha za pembe tatu kwa pamoja kisha uanze kuipitisha juu ya bakuli au sufuria yenye mafuta yaliyozidi.

Tishu ina uwezo mkubwa wa kunyonya mafuta kama utaipitisha kwa juu kiasi kwamba mchuzi au maji hayataingia.

Unaweza kubadilisha tishu ukihisi imejaa. Rudia hatua hiyo mpaka utakaporidhika na kiwango cha mafuta yaliyopo.

Njia hii ya kupunguza mafuta kwwa njia ya karatasi za tishu inafaa sana wakati mboga imepoa na mafuta yamejitenga. Picha|Pinterest.

Kupunguza mafuta kwa kutumia kijiko chenye barafu

Kwenye mbinu hii unachotakiwa kufanya ni kuweka vipande vya barafu kwenye kijiko kikubwa cha chakula na kukipitisha juu ya mchuzi au supu yako kisha kifute kwa pembeni kwenye tishu au kitambaa kisafi

Kijiko chenye barafu kinapopitishwa juu ya mafuta kinagandisha tabaka la juu la mafuta hivyo kuacha mboga yako ikiwa haina mafuta.

Kupunguza mafuta wa kutumia kijiko

Kama una haraka mbinu hii itakufaa zaidi

Ikiwa una supu au mchuzi mwingi ni vyema kutumia kijiko kikubwa cha mchuzi kurahisisha upunguzaji mafuta kwenye mboga au supu.Picha|Went here 8 this.

Unachotakiwa kufanya ni kuchota mafuta yaliyozidi kwa kutumia kijiko cha chakula.

Hata hivyo, njia hii haitapunguza mafuta kwa kiwango kikubwa kwa sababu ni rahisi sana mafuta kuchanganyika na maji wakati unachota hivyo kupunguza mchuzi badala ya mafuta.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa