Pilau ni moja kati ya chakula maarufu kinachopikwa na kuliwa kwenye matukio maalumu kama sikukuu na sherehe mbalimbali.
Harufu nzuri itokanayo na viungo vinavyowekwa kwenye chakula hiki huongeza hamu kwa walaji, majirani na wapita njia wa sehemu chakula hiki kinapoandaliwa.
Licha ya umaarufu wa chakula hiki aina za mapishi yake hazifanani kuna pilau la viungo, pilau nyama, pilau nazi, pilau maharage na pilau bubu ambalo linapikwa bila nyama.
Aina zote hizo zinathibitisha msemo wa wahenga usemao ‘mchele mmoja mapishi mbalimbali’. Kwa siku ya leo tuuthibitishe msemo huu kwa kujifunza mapishi ya pilau la viungo na nyama ya ng’ombe.
Utamu wa Pilau la viungo na nyama ya ng’ombe
Aina hii ya pilau ni ile iliyokuwa inatumika miaka kadhaa nyuma na linahusisha aina nyingi za viungo. Awali viungo hivyo ambavyo vilikuwa vinawekwa vizima vizima kwa pamoja bila kutwangwa.
Licha ya kuonekana kupitwa na wakati mpaka leo bado aina hii ya upishi inavutia wapishi wengi hata walimu wa mapishi kwenye madarasa mbalimbali ya mapishi mtandaoni.
“Siwezi kupika pilau bila kuweka viungo ambavyo havijatwangwa, hata ukifuatilia madarasa yangu yote ya mapishi… najua msingi wa pilau upo kwenye viungo vingi,” anasema Latifa Mohamed mmoja wa wakufunzi katika darasa la mapishi la ‘Recipe’ linalofanyika kupitia mtandao wa WhatsApp.
Maandalizi
Maandalizi ya pilau hili lenye viungo huanza kwa kukatakata nyama kuosha, kusagia tangawizi na kitunguu swaumu kisha kuichemsha mpaka iive.
Wakati unasubiri nyama iive andaa viungo vingine kama njegere, viazi kitunguuu saumu, mdalasini, binzari nyembamba, pilipili manga, karafuu na hiriki.
Ukimaliza kuandaa viungo anza mapishi kwa kubandika sufuria weka mafuta kiasi, kaanga vitunguu maji hadi viwe vya kahawia kisha weka tangawizi, kitunguu saumu na ukoroge kwa dakika kati ya mbili hadi tatu inategemeana na uwingi wa chakula. Hii itasaidia vichanganyike vizuri na mafuta.
Ongeza binzari nyembamba, iriki na karafuu kisha weka nyama na ukoroge ichanganyike na viungo kwa dakika tano.
Wakati huo ukiendelea kukoroga weka nyanya mbili ulizokata vipande vidogovidogo, weka karoti na maharage machanga kisha malizia kwa kuweka soya sauce na chumvi kiasi.
Ukiridhika na kiwango cha chumvi uliyoweka ongeza mchele na ukoroge kwa dakika tano kabla ya kuongeza mahitaji na viungo vingine.
Zingatia haya
Kwenye hatua hii Latifa anasema huwasisitiza wanafunzi wake kuongeza bidii kwenye kuchanganya mchele ili viungo vikolee vizuri.
“Ukizembea kwenye hatua hii basi pilau lako halitanoga…kadri unavyochanganya ndio jinsi pilau lako litatoka tamu zaidi zingatia tu usiunguze,” anasema Latifa.
Baada ya dakika tano weka maji kiasi, supu ya nyama na viazi kisha ufunike uache pilau liive kwa moto mdogo.
Kwenye hatua hii wengine hupenda kupalia moto wa mkaa kwa juu lakini kwa mapishi ya nishati safi kama gesi na umeme hakuna haja ya kupalia.
Baada ya dakika 30 au 45 geuza pilau lako na uongeze zabibu kavu kiasi kisha uache liive kwa dakika 20 na litakuwa tayari kuliwa.
Maandalizi ya Kachumbari
“Pilau halinogi bila kachumbari,” anasema Neema John, mkazi wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Mama huyo maarufu kama mama Mahiri anaeleza kuwa kachumbari nzuri ni ile yenye mchanganyiko wa mahitaji mengi ambayo yana faida zikiwemo za kiafya.
Zingatia kugawa kachumbari isiyo na pilipili iwapo una wanafamilia wasiotumia kiungo hicho.
Maandalizi yake ni ya kawaida ambayo huanza kwa kumenya na kukatakata kitunguu kisha unaokiosha na maji na kukiweka kwenye bakuli safi.
Kata nyanya na tango kwa saizi ndogo ndogo na uweke kwenye bakuli lenye vitunguu.
Baada ya hapo menya parachichi na ulikate kwa vipande vidogo vidogo, hakikisha halijaiva sana wala kurojeka. Changanya viungo vyote na uongeze chumvi, vijiko viwili vya maji ya ndimu na pilipili kiasi.
Mpaka hapo kachumbari yako ipo tayari kwa kuliwa na pilau huku ikisindikizwa na kinywaji chochote ukipendacho.