Mtori ni moja kati ya chakula maarufu kinachotumika zaidi wakati wa asubuhi kwa watu wazima au watoto.
Chakula hiki kimejizolea umaarufu mwingi sehemu mbalimbali nchini, huku kikisindikizwa na vitafunwa mbalimbali kama chapati na maandazi.
Kwa watoto wadogo, wagonjwa na wazazi waliotoka kujifungua chakula hiki kimekuwa sehemu ya mlo wao wa siku unaowapatia nguvu na ladha ya kipekee.
Kuna aina mbalimbali za mapishi ya chakula hiki. Mapishi ya mtori kwa kutumia kipekecho (kifaa cha asili kinacho tumika kusaga chakula), blenda au kusaga kawaida na mwiko.
Leo tutajifunza aina hizo tatu rahisi ambazo unaweza kupika nyumbani na ukaachana na habari ya kununua mgahawani au hotelini.
Tuingie jikoni sasa
Maandalizi ya awali ya pishi hili ni pamoja na kuandaa nyama kwa kuikata kata na kuisaga, kitunguu swaumu, tangawizi na jiko la kisha ubandike na uache iive.
Wakati unasubiri nyama kuiva andaa ndizi kwa kuzimenya na kuziosha, kitunguu maji, karoti, hoho, maji ya ndimu na nyanya kama utapendelea.
Baada ya hapo chemsha ndizi zako mpaka ziive tayari kwa kuandaa mtori.
Mtori wa kusaga kwa kutumia kipekecho
Mara baada ya nyama na ndizi kuiva anza kwa kuweka ndizi kwenye bakuli safi au sufuria kisha uziponde ndizi kwa kipekecho taratibu na kuondoa mabonge yote.
Baada ya hapo anza kusaga kwa kupekecha taratibu huku unaongeza supu ya nyama taratibu mpaka ndizi zako zilainike kabisa.
Rudia hatua hiyo mpaka uridhishwe na ulaini wa mtori wako kisha rudisha jikoni ongeza supu iliyobaki,mafuta ya kupikia chumvi, kitunguu, karoti hoho na uache uive kwa dakika tano na mtori wako utakuwa tayari.
Mtori wa kusaga na blenda
Aina hii ya mapishi inafaa sana kwa watu wenye haraka, unachotakiwa kufanya ni kuweka ndizi zako zilizoiva kwenye blenda, ongeza supu na usage mpaka zilainike.
Hakikisha ndizi zako zimepoa ndipo usage pia uweke kidogo kidogo ikiwa una ndizi nyingi.
Baada ya hapo mimina mchanganyiko wako kwenye sufuria ongeza supu iliyobaki,mafuta ya kupikia kiasi, chumvi, kitunguu, karoti hoho na uache uive kwa dakika tano na mtori wako utakuwa tayari kwa kuliwa
Mtori wa kusaga na mwiko
Hapa pia hakuna mambo mengi ni kuponda tu ndizi kwenye sufuria kwa kutumia mwiko mpaka mabonge yote yaishe.
Rudia tena kuponda huku ukiongeza supu taratibu mpaka iwe laini kabisa kwa kiwango unachotaka.
Ukiridhishwa na ulaini huo basi rudisha jikoni pika kwa moto mdogo kwa dakika 5 ongeza supu iliyobaki, mafuta ya kupikia kiasi na viungo vingine vyote kisha unaweza kutenga.