Hatua kwa hatua: Jinsi ya kupika matoke ndani ya muda mfupi

Na Lucy Samson
24 Aug 2022
Ni miongoni mwa vyakula vinavyopendwa zaidi mkoani Kagera na unaweza kukipika ndani ya dakika 30.
article
  • Pishi hili linatumia dakika 30 kukamilika 
  • Kama hauna kinywaji kama sharubati unaweza ukashushia na maji tu fresh. 
  • Hutakiwi kugeuza pishi hilo kwa kuwa ndizi ni laini na samaki atavurugika. 

Hapana shaka uliwahi kusikia chakula mashuhuri kutoka mkoani Kagera kiitwacho Matoke. Chakula hiki ni sehemu ya ‘menu’ ambayo huwezi kuikoa kwa watu wa kabila la Wahaya.

Kwa jamii hii iliyopo kaskazini magharibi mwa Tanzania, chakula hiki kinaaminika kuwa ni cha heshima sana na huliwa na watu wa rika zote.

“Yani mgeni hawezi kuja kwako ukaacha kumpikia matoke hata kama huna ndizi nyumbani ni heri ukanunue,” anasema Liberatha Respicius aliyenifundisha kupika pishi hili.

Liberatha anasema chakula hiki kiasili kabisa kinaitwa “Ebitoke” yaani chakula cha ndizi ambacho hupikwa pamoja na maharage, nyama au samaki. Naam Ebitoke, ila siyo yule mwigizaji unayemfahamu. 

Mahitaji

Ili kupika pishi hili la Kihaya ni lazima uwe na mahitaji yafuatayo ambayo yatategemea idadi ya watu watakao kula mlo huo.

  • Ndizi hususan ndizi Bukoba
  • Maharage 
  • Samaki mbichi au aliyekaangwa (Sato anafaa zaidi kama anapatikana kirahisi)
  • Nyanya 
  • Kitunguu kimoja
  • Mafuta chumvi na karoti.

Maandalizi

Menya ndizi na uzioshe vizuri, chambua maharage uyaoshe na kubandika jikoni mpaka yaive.

Maharage yakiiva weka ndizi ulizomenya na kuzikata kata, ongeza kitunguu, nyanya, chumvi na mafuta kisha uweke samaki kwa juu na maji kiasi na ufunike ili ziive.

Ukienda kwenye jamii ya Wahaya utaona wanatumia majani ya migomba kama mifuniko hapa Liberatha anatueleza umuhimu wa kutumia mifuniko hii ya asili.

Matoke yanaweza kupikwa na nyanya chungu ili kuongeza ladha na Vitamini. Picha|Bukoba Wadau/Facebook

“Ukifunika kwa kutumia majani ya migomba chakula kinaongezeka ladha na kuwa kitamu,pia majani ya migomba hutumika kama sahani wakati wa kula,” anasema Liberatha. 

Baada ya muda funua na uangalie ndizi zako kama zimeiva kama bado ufunike tena.

“Ndizi hizi ni laini sana ukizigeuza mara kwa mara zitapondeka hivyo nashauri mtu akitaka kuzipika aweke tu moto mdogo zinaiva bila kugeuza,” anasema Liberatha na kuongeza kuwa hata samaki zitaiva bila kugeuzwa.

Inatarajiwa pishi hili litakuwa limeiva ndani ya dakika 30.  

Ukijiridhisha kama ndizi zako zimeiva na kiwango cha mchuzi kinatosha hapo ndizi zako zitakuwa tayari kabisa kwa kuliwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa