Zege la tambi za mayai ni moja kati ya aina mpya ya chakula inayojizolea umaarufu kwa kwa baadhi ya wapishi wasiopenda kukaa muda mwingi jikoni.
Ikiwa utakula chakula hiki kwa mara ya kwanza pasi na shaka unaweza kudhani ni chipsi mayai au ‘zege’ kama wengi wanavyopenda kuliita.
Kuanzia maandalizi,muda wa kuandaa na muonekano wake kwa ujumla pishi hili linafanana sana na pishi la chipsi mayai.
Kwa wauzaji wa hoteli,migahawa na ‘mama ntilie’ wanaweza kuongeza pishi hili linaloweza kuwaongezea wateja wanaokipenda chakula hicho.
Tusogee jikoni tujifunze mbinu rahisi za kuandaa ‘zege’ la tambi mayai.
Maandalizi
Mapishi yetu ya tambi za mayai yanaanza kwa kuandaa kuchemsha maji kiasi kwa ajili ya kuchemshia tambi kabla ya kuzikaanga na mayai.
Maji yakichemka weka tambi na uziache jikoni kwa dakika 3 mpaka 5 kutokana na wingi wa tambi zako. Baada ya hapo zichuze na uziache wazi zipoe.
Hatua inayofuata ni kuandaa mayai kwa kuyapasua na kuyakoroga mpaka yachanganyike vizuri, kisha menya nyanya,kitunguu na hoho utakavyo vitumia katika pishi lako.
Baada ya kumaliza maandalizi hayo changanya tambi ulizozichemsha, chumvi kiasi na viungo vyote ulivyoviandaa. Hakikisha vimechanganyika vizuri kabla ya kuweka jikoni.
Bandika kikaango weka mafuta kiasi ikifuatiwa na tambi pamoja na viungo ulivyochanganya, mimina mayai kwa juu (kama unavyomimina wakati wa kukaanga chipsi mayai) kisha acha yaive.
Baada ya dakika tatu geuza tambi taratibu kwa kijiko kipana ili zege lako lisivurugike kisha acha upande huo uive kwa dakika mbili nyingine.
Ili zegelako liive vizuri tumia kijiko kusukuma kwa juu ili kuruhusu sehemu ya ndani ya tambi na mayai kuiva.Hatua hii pia itasaidia tambi kukauka vizuri.
Mpaka hapo pishi lako lipo tayari kwa kula unaweza ukasindikiza na soda, juisi au chai.