Kuna wanaodhani samaki makange wa kupika nyumbani sio mtamu kama wale wanaopatikana hotelini, migahawani au kwa mama ntilie.
Leo tumekuletea maujanja ya kupika samaki makange nyumbani na ladha yake ifanane na ladha ya migahawani au hotelini.
Samaki makange anaweza akaliwa na ugali, wali, tambi au chipsi ila leo tutaandaa samaki makange atakayeliwa na wali maua.
Maandalizi
Hatua ya kwanza ni kuosha samaki na kumuandaa kwa ajili ya kumkaanga. Hapa unaweka tangawizi, kitunguu swaumu, ndimu kiasi na masala.
Kisha funika samaki wako na umuache kwa dakika 10 mpaka 20 ili viungo viingie ndani ya samaki vizuri.
Wakati unasubiri viungo vienee kwenye samaki unaweza kupika wali, kwa kuanza na kuchambua mchele kuosha hoho na karoti kisha ukate kwa saizi ya boksi ili kuleta muonekano mzuri. Menya njegere na uzioshe.
Washa jiko na uchemshe maji ya moto utakayoyatumia kupika wali, yakichemka weka sufuria nyingine jikoni, ongeza mafuta kiasi utakayoyatumia kukaanga viungo vya kupika wali.
Mafuta yakipata moto weka vitunguu na ukaange mpaka viwe vya rangi ya kahawia kisha ongeza karoti na njegere na ukaange kwa muda. Malizia kwa kuongeza maji kiasi yatakayotosha kuivisha wali.
Yakichemka ongeza chumvi kiasi, na uongeze mchele uliochambua na kuosha vizuri mwanzoni. Funika uache uive wa moto mdogo.
Wakati wali unaiva tuandae makange yetu sasa.
Weka mafuta jikoni yakichemka mkaange samaki wako kwa moto mdogo mpaka awe na rangi ya kahawia, wakati ukisubiri samaki aive unaweza kuosha nyanya, kitunguu, karoti na hoho kwa ajili ya kuunga samaki akiiva.
Saga nyanya na karoti kwenye brenda au unaweza kusaga kwenye kisagio cha mkono, hoho na karoti nyingine ukate kwa saizi ya urefu ili vilete muonekano mzuri wa makange yako.
Samaki akiiva vizuri, weka sufuria nyingine jikoni na ukaange vitunguu, weka nyanya na karoti uliyosaga na uache vichemke.
Weka samaki wako kisha ufunike kwa dakika tano baada ya hapo ongeza chumvi, ndimu na viungo vingine vilivyobakia. Hakikisha mchuzi unakuwa mzito na uongeze pilipili kama unapendelea.
Weka tui la nazi au nazi ya pakti ili kuongeza ladha zaidi. Samaki makange sasa ipo tayari kuliwa na wali wa maua.