Wachaga wana vyakula vingi vya kiutamaduni ambavyo huliwa kwenye matukio mbalimbali. Kuna mtori, ngararimo, kitawa, ng’andi, kiburu na vingine vingi kutegemea na ukanda mpishi anapotokea.
Nimemtembelea Jojina Kinabo (mama Diana) anayeishi jijini Dar es Salaam ambaye amenifundisha jinsi ya kupika ng’andi za kichaga, nimeona nikuletee na wewe ujuzi huu uweze kubadilisha menyu lakini pia uweze kuonja ladha hii ya kipekee ya watu wa kaskazini.
Ng’andi ni jina la kichaga lenye kumaanisha chakula cha ndizi na maharage kilichosongwa. Mahitaji ya chakula hiki ni ndizi maharage,mafuta ya kupikia, kitunguu, karoti, hoho na magadi.
Chakula hiki kina mahitaji machache na ni rahisi kukipika, tukaribie jikoni tupike ng’andi.
Maandalizi
Menya ndizi, zioshe na uzikate kwa saizi ndogo ndogo, chambua maharage na uyaoshe tayari kwa ajili ya kuyabandika.
Mimi nimeyaloweka maharage yangu kwa masaa 12, ili iwe rahisi kuyapika kwenye gesi.
Mama Diana aliiniambia enzi zao walikuwa wanapikia kuni tena kwenye chungu ilichukua saa nne mpaka matano kuivisha chakula hiki.
“Heri yenu sasa hivi kuna gesi mnapika kwa haraka, tofauti na enzi zetu” anasema mama Diana.
Baada ya kuchemsha maharage, yakishaiva weka ndizi kwa juu na maji kidogo mpaka ziive.
Ongeza na magadi au “mbaala” kama unavyoitwa kwa kichaga
Zikiiva anza kuzisonga taratibu bila kugusa maharage ya chini, zikisagika zichanganye na maharage kwa kuzikoroga kwa pamoja na maji kiasi.
Kwenye sufuria ya pembeni kaanga kitunguu, karoti na hoho kisha uweke mchanganyiko wako wa ndizi na maharage.
Funika kidogo zichemke, ukihakikisha maji yamekauka na kubaki na mchuzi mzito hapo ng’andi zako zitakuwa tayari.
Mbali na chakula hiki kuliwa na watu wa rika zote, chakula hiki kina protini nyingi yenye kujenga mwili.