Njia rahisi ya kupika ‘egg chop’ za nyama

Na Fatuma Hussein
1 Jul 2024
‘Egg chop’ huenda kwa baadhi ya watu ni jina geni kwa kuwa si kitafunwa maarufu kati ya vile vilivyozoeleka katika maisha ya kila siku ya mwananchi wa kawaida kama maandazi, chapati au vitumbua. Kama wewe ni miongoni mwao ondoa shaka, Jiko Point itakusaidia kukutoa tongotongo kwa kuwa leo tunakwenda kujifunza jinsi ya kuandaa kitafunwa hiki […]
article
  • Unaweza kuandaa nyumbani kwa ajili ya familia.
  • Itakupunguzia gharama ya vitafunwa na kufungua fursa ya biashara.

‘Egg chop’ huenda kwa baadhi ya watu ni jina geni kwa kuwa si kitafunwa maarufu kati ya vile vilivyozoeleka katika maisha ya kila siku ya mwananchi wa kawaida kama maandazi, chapati au vitumbua.

Kama wewe ni miongoni mwao ondoa shaka, Jiko Point itakusaidia kukutoa tongotongo kwa kuwa leo tunakwenda kujifunza jinsi ya kuandaa kitafunwa hiki kitamu unachoweza kukiandaa nyumbani kwako na kufurahia wewe na familia yako.

Nikujuze tu bei ya egg chop katika migahawa  huuzwa kati ya Sh1,000 hadi Sh1,500 kulingana na aina ya mgahawa ingawa baadhi ya maeneo bei yake inafikia Sh2,000 mpaka Sh2,500.

Hivyo ukiandaa pishi hili utakuwa umeokoa gharama lakini pia itakuwa umepata fursa ya biashara ya kitafunwa hiki mtaani kwako.

Mahitaji ya egg chop za nyama

Nyama ya kusaga na hii inaweza kuwa nyama ya aina yoyote ile ya kuku, mbuzi ama ngo`mbe kutegemeana na chaguo la mpishi au walaji, pia zipo egg chop zisizowekwa nyama.

Kitunguu saumu na tangawizi iliyosagwa, pilipili manga ya unga, au pilipili ya kawaida iliyosagwa, uzile au binzari nyembamba pamoja na kotmiri au korienda (ingawa sio lazima).

Mkate wa slesi uliosagwa au bread crumbs, hii kama huwezi kununua unaweza kutengeneza mwenyewe nyumbani kwa kuukausha mkate wako juani au kwa kutumia ‘microwave’ kisha ukausaga na mambo yakawa sawa kabisa.

Mayai ya kuchemsha kiasi kitakachokutosha wewe na familia yako kwa ajili ya kuchanganyia nyama pamoja na mayai ya kuchomea.

Namna ya kuandaa chakula chako

Hatua ya kwanza ni kuchemsha mayai uliyokadiria kwa wastani wa dakika 10 mpaka 15 kisha uyatoe maganda.

Baada ya hapo changanya nyama iliyosagwa na viungo , kisha uiweke kwenye kikaango kwa ajili ya kuikausha kwa muda wa dakika 10 mpaka 15 na baada ya hapo utaisaga kidogo kwenye blender ili upate mchanganyiko mzuri.

Utaongeza mikate iliyosagwa pamoja na mayai kwenye huo mchanganyiko wa nyama na viungo.

Mara baada ya kuhakikisha umechanganya vizuri mchanganyiko sasa utachukua mayai yaliyochemshwa na utazungushia mchanganyiko huo kwa umbo la duara.

Hatua ya mwisho ni kukoroga mayai mengine ambao utatumika kama gundi ya kuzuia mchanganyiko kuvurigika wakati unaweka kwenye mafuta kwa ajili ya kukaanga.

Kaanga egg chop kwa moto wa wastani mpaka zitakapobadilika na kuwa na rangi ya kahawia kisha utaipua na kuziacha zipoe kwa dakika tano ndipo uzikate.

Kumbuka tu pishi hili ni rahisi kufuata na linafaa kwa wapishi wa viwango vyote, na matokeo yatakuacha na shauku ya kutaka kujifunza zaidi na zaidi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa