Njia rahisi ya kupika kachori za viazi nyumbani

Na Mariam John
8 Jul 2022
Kitafunwa hiki ambacho kinakuwa na mchanganyiko wa unga wa ngano, viazi mviringo, manjano, pilipili na chumvi unaweza kupika kwa haraka kwenye jiko la gesi au umeme.
article
  • Unaweza kuandaa nyumbani
  • Mahitaji ni unga wa ngano, viazi mviringo, manjano, pilipili, chumvi na mafuta ya kupikia.
  • Unaweza kutumia asubuhi au jioni.

Kila mtu ana aina yake ya kitafunwa ambacho anakitumia kama kifungua kinywa wakati wa asubuhi. Wapo wanaotumia maandazi, chapati, mikate au hata mihogo. 

Matumizi ya vyakula hivyo hutegemea urahisi wa upatikanaji wake lakini uwezo wa kuvitengeneza kwa sababu vingine huchukua muda kuviandaa.

Leo tunajifunza namna ya kuandaa kachori. Kitafunwa hiki kimekuwa kikitumiwa na watu wengi hasa wanafunzi shuleni. Kama hujawahi kukitumia, basi baada ya kusoma makala hii utakua mdau muhimu wa chakula hichi.

Kitafunwa hiki kinaweza kuandaliwa na kikawa tayari kwa muda wa dakika 30 hadi 45 na itategemea na aina ya nishati unayotumia. Ukitumia jiko la gesi au umeme hakichukui muda mrefu kuiva.

Mahitaji

Ili kuweza kupika chakula hiki vitu vifuatavyo vinapaswa kuandaliwa:

  1. Viazi mviringo (kilo moja au nusu kilo)
  2. Unga wa ngano (robo kilo)
  3. Pilipili ya unga (kijiko kimoja)
  4. Unga wa manjano
  5. Mafuta ya kupikia (chupa moja)
  6. Vitunguu saumu, hoho na chumvi.

Namna ya kuandaa

Menya viazi vyako kisha vichemshe hadi viive kabisa.  Baada hapo viipue kisha weka kwenye bakuli lako safi na uviponde ponde au unaweza kuvisaga kwenye blenda vilainike.

Hakikikisha hakuna mabonge bonge kwenye viazi vyako.

Chukua unga wako wa ngano, changanya na manjano, pilipili, vitunguu saumu ambavyo tayari vimesagwa na chumvi kwa ajili ya kupata ladha. Weka kwenye bakuli kwa pamoja na changanya kisha koroga kuhakikisha unapata uji mzito. 

Baada ya zoezi hilo, chukua viazi vyako ambavyo tayari umeviponda ponda na utengeneza madonge kiasi unachopendelea.

Madonge hayo yachovye kwenye unga wa ngano kisha tumbukiza kwenye mafuta ambayo tayari yatakuwa yamechemka na kaanga hadi uone yameanza kubadilika rangi.

Usiweke madonge yote kwenye mafuta kwa wakati mmoja bali weka kulingana na wingi wa mafuta yako. Ikikamilisha vitoe kwenye mafuta na weka kwenye sahani safi tayari kwa kuliwa.

Unaweza kutumia kitafunwa hiki kwa chai au juice. Unaweza kukitumia asubuhi au jioni hasa kwa wale ambao hawapendi kula chakula kizito.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa