Njegere ni miongoni mwa nafaka zinazofahamika sana nchini Tanzania kwa uzuri wake wa kunogesha aina yoyote ya chakula utakayoweza pika kwa wakati wowote iwe asubuhi, mchana, jioni au usiku.
Mboga hii hutumiwa katika aina nyingine za mapishi kama pilau, wali na hata kwenye aina kadha za tambi.
Njegere hunoga zaidi zikipikwa na nyama ya ng’ombe, nyama ya kuku au aina yoyote ya nyama utakayoipendelea.
Mbali na njegere za nazi tulizozioea leo tutaandaa njegere za nyama ya kuku ambazo zinaweza kupikwa nyumbani, kwenye sherehe au sehemu ya biashara.
Kwa mabachela au wanaotaka kubana bajeti mboga hii inaweza kuwa mbadala wa maharage au mboga nyingine zilizozoeleka.
Maandalizi
Mapishi yetu leo yanaanzia gengeni ambapo unaweza kupata mahitaji yote kwa bei rahisi kutegemea na mazingira uliyopo.
Katika masoko au magenge mengi njegere huuzwa kuanzia Sh1,000 na kuendelea, bei inaweza kutofautiana ikiwa utanunua maeneo kama ‘Super market’ ambapo bei inaweza kuongezeka zaidi.
Mahitaji mengine kama kuku unaweza kununua kiasi chako, kibachela bachela unaweza kununua vipande vya kuku kibandani kuanzia Sh 1,000 na ukaendelea na mapishi yako.
Nunua nyanya kubwa moja kwa Sh200, nazi ya pakti kwa Sh1,000, kitunguu maji, kitunguu swaumu, karoti, pilipili hoho, mafuta na chumvi kisha uviandae kwa mapishi.
Baada ya kuhakikisha umeandaa mahitaji yote kwa kuosha na kukatakata endelea kwa kuchemsha njegere kwa muda wa dakika 15 hadi 20.
Baada ya hapo chemsha na ukaange kuku tayari kwa kuunga, kama ulinunua kuku aliyekaangwa basi utaruka hatua hii.
Anza kuunga mboga yako kwa kuwasha jiko, Kisha bandika sufuria na ukaange kitunguu swaumu kikifuatiwa na kitunguu maji na upike mpaka vilegee na kutoa manukato.
Ongeza nyanya, chumvi na viungo vya mchuzi kama ‘curry powder’ au vingine unavyopendelea.
Subiri kwa muda wa hadi dakika sita ili viungo viive ipasavyo, baada ya hapo weka njegere na kuku kisha ongeza maji, kukoroga na uache viive.
Baada ya dakika tatu weka chumvi, karoti, hoho na tui la nazi kisha utakoroga kwa pamoja hadi mboga yako itakapokuwa tayari.
Kama unatumia nazi ya kukuna tenganisha tuu la kwanza na la pili kisha anza kuweka tui la mwisho na likichemka kidogo ongeza la kwanza huku ukiendelea kukoroga.
Katika hatua hii usifunike sufuria ili kuzuia tui kukatika na kuharibu muonekano wa mboga unayoiandaa.
Ikichemka na ukaridhishwa na uzito wa mchuzi, njegere zako zitakuwa tayari, unaweza kuongeza pilipili kama utapendelea.
Kuwa huru kula mboga hii pamoja na aina yoyote ya chakula kama wali, ugali, pilau, chipsi, ndizi za kukaanga, mkate au chapati.