Kwa familia zinazopenda kukaangiza vyakula, huenda mafuta ikawa ni kati ya vitu vinavyomaliza fedha nyumbani.
Kama wali ni wa kukaanga, samaki ni wa kukaanga, nyama ni ya kukaanga na mboga mboga nazo ni za kukaanga, ni wazi kuwa mafuta ya kupikia hayawezi kukaa kwa muda mrefu nyumbani hapo.
Ili kupunguza matumizi ya mafuta katika kaya yako, yapo baadhi ya mambo unayoweza kuzingatia ikiwemo kujisasisha kwa teknolojia.
Hizi ni baadhi ya njia unazoweza kutumia kupunguza matumizi makubwa ya mafuta nyumbani.
Toa elimu kwa wapishi
Chakula kitamu wala siyo lazima kiwe kimepikwa kwa mafuta mengi. Unahitaji mafuta kiasi kupika wali, mboga ya majani na hata nyama.
Kama mlezi wa familia, ni muhimu kutoa elimu kwa wanaohusika jikoni na ikiwezekana utoe elimu hiyo kwa mfano.
Mfanyabiashara wa bidhaa za jumla kutoka Shinyanga, Daye Benjamin amesema mwanzoni mke wake alikuwa akitumia mafuta mengi katika mapishi. Aliamua kuongea naye ili kiasi kinachotumika kipungue.
“Unakuta chupa moja inachukua siku tatu tu. Niliona nimwambie sipendi vyakula vyenye mafuta mengi, Alipunguza na sasa chupa inaweza kumaliza hata wiki,” amesema Benjamin.
Tumia teknolojia za kisasa
Teknolojia imeshabadilika. Kwa sasa mtu ana uwezo wa kukaanga nyama kwa matone kadhaa tu ya mafuta.
Mashine ya Air Fryer ambayo mtu anaweza kupika chakula chochote hata chipsi kwa kutumia kijiko kimoja cha mafuta na chakula kinakuwa tayari kwa ajili ya kutumiwa.
Zingatia mafuta kwenye mboga unazonunua
Kuna baadhi ya mboga hasa nyama, huwa zina mafuta. Kwa mboga kama hizo, hauna ulazima wa kuweka mafuta mengi wakati unapika.
Mkazi wa Kinyerezi, Flavian Kanyira amesema kujua aina ya nyama unayoinunua ni kukomboa gharama zingine.
Yeye anapenda kununua nyama ya nundu kwa kuwa anapenda kukaanga nyama.
“Nikiichemsha ile, inakuwa na mafuta ya kutosha tu. maji yakikauka, mafuta yanabaki natumia hayo hayo kukaangia nyama na kuungia viungo,” amesema Kanyira.
Fahamu ya kuwa, wataalam wa afya wanatahadharisha kuwa matumizi makubwa ya mafuta ya kupikia kwenye vyakula yanaweza kumuweka mtu katika hatari ya kupata uzito uliopitiliza, magonjwa ikiwemo ya moyo, kiharusi na saratani.
Daktari wa mafunzo wa tiba katika Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Cha Muhimbili (Muhas), Edrick Mwaipinga aliwahi kuiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, kila mtu kutokana na mwili wake kuna kiwango stahiki cha mafuta kinachohitajika, lakini visizidi vijiko viwili kwa siku.
Amesema matumizi ya teknolojia zinazodhibiti matumizi makubwa ya mafuta ni moja ya njia zinazoweza kutumika kuepukana na magonjwa yatokanayo na matumizi makubwa mafuta mwilini.
“Kila mtu ana kiwango chake cha mafuta kinachohitajika mwilini bila kuzidi kiasi cha vijiko viwili kwa siku hii ni kutokana na maumbile aliyonayo mtu,” aliwahi kusema Dk Mwaipinga.