Mahindi ni miongoni mwa vyakula vyenye mapishi mengi, yanaweza kuliwa yakiwa mabichi baada ya kuchemshwa, kuchomwa, kukaangwa, kupikwa kama kande pamoja na kutumika kutengeneza unga wa ugali.
Ukiachana na mapishi hayo yaliyozoeleka kwenye jamii nyingi hii leo kwenye Jiko Point tunakwenda kutizama pishi jipya la mahindi, ambayo ni mahindi ya kuunga na nazi au maziwa.
Tuingie jikoni
Hatua ya kwanza ni kuchemsha mahindi (unaweza kuchemsha mazima au kwa vipande vidogo vidogo) mpaka uhakikishe yameiva vizuri kwa mahindi machanga unaweza kutumia dakika 15 -20 ukipata mahindi magumu unaweza kutumia dakika 30 – 45
Baada ya hapo katakata kitunguu maji na nyanya vipande vidogo vidogo kisha weka mafuta katika sufuria, yakipata moto tia vitunguu, kaanga kwa dakika 1 mpaka vianze kuwa laini ndio uweke nyanya.
Hatua inayofuata saga karoti tia kwenye mchanganyiko na ukate kate mahindi vipande vitakavyo kuvutia kisha uweke kwenye mchanganyiko, tia chumvi kisha koroga vizuri na uache jikoni kwa dakika tano mpaka 10.
Ukimaliza hatua hiyo tia tui la nazi liache kwa dakika 3 kisha malizia kwa kuweka majani ya kortimili kwa juu na chakula kitakuwa tayari kwa kuliwa.
Vitu vya kuzingatia
Mahindi yanatakiwa ya chemshwe kwanza yawe ni mateke na sio makavu pia unaweza kuchanganya mbogamboga upendazo au kitoweo ukipendacho.