Kama bado unajiuliza ni kitafuwa gani unaweza kuongeza katika mgahawa au sehemu yako ya biashara ili uendelee kunasa wateja, kachori za nyama zinaweza kuwa jibu lako.
Wakati kachori ya kawaida ikiuzwa kwa Sh200 mpaka 500, ukiongeza mayai unaweza kuuza kuanzia Sh1,000 hadi Sh2,000 kutegemea na eneo utakalouzia.
Kachori hizi pia zinaweza kupikwa nyumbani na kupunguza gharama ya kununua vitafunwa kwa ajili ya kifungua kinywa.
Mapishi yake hayatofautiani sana na yale ya kachori za kawaida, hapa utahitaji mayai yaliyochemshwa ili kuongeza ladha zaidi.
Sogea jikoni
Kama ilivyo katika mapishi ya kachori za kawaida, tutaanza kwa kuandaa viazi kwa kuvimenya, kuvikataka na kuviosha vizuri na maji safi.
Baada ya hapo chuja maji na uvichemshe jikoni viive taratibu kwa moto mdogo mdogo, usiviache jikoni kwa muda mrefu mpaka vikarojeka.
Viazi vikiiva vitoe kwenye maji na uviweke kwenye bakuli safi kisha uviponde mpaka vilainike. Unaweza kutumia mwiko au kifaa maalum cha kupondea (masher).
Kwenye bakuli ya viazi unaweza kuongeza vitunguu maji, karoti, hoho, maji ya limao, chumvi na pilipili kama unapendelea kisha changanya vizuri.
Hatua hiyo ikikamilika, hamia kwenye kuchemsha mayai mpaka yaive kisha bandua maganda na uyagawe mara mbili kwa kukata kati kati. Inamaana kama una mayai manne utapata vipande nane.
Kutengeneza umbo la kachori utachukua viazi vilivyopondwa kidogo mkononi utaweka yai lililokatwa nusu kisha utalifunika na kiasi kingine kidogo cha viazi na kutengeneza duara.
Endelea na mapishi kwa kumimina kiasi kidogo cha unga kwenye bakuli safi, ongeza chumvi kiasi, rangi na maji ili utengeneze mchanganyiko mzito, anza kupitisha donge moja moja kwenye mchanganyiko huo.
Baada ya kupita kwenye mchanganyiko huo tumbukiza kwenye mafuta ambayo tayari yatakuwa yamechemka na kaanga hadi uone yameanza kubadilika rangi.
Usiweke madonge yote kwenye mafuta kwa wakati mmoja bali weka kulingana na wingi wa mafuta yako. yakiiva yatoe kwenye mafuta na weka kwenye sahani safi tayari kwa kuliwa.