Unavyoweza kupika biriani ya nyama

Na Lucy Samson
5 Jul 2022
Ili upike biriani hii unatakiwa kuwa na mahitaji yote ikiwemo mchele, nyama ambavyo utavipika tofauti.
article
  • Hakikisha una mahitaji yote ikiwemo nyama na wali.
  • Fuata hatua zote za upishi.

Bado kuna maoni tofauti juu ya asili ya chakula cha biriani. Wapo wanaosema kimetokea Uajemi, wengine wanasema kimetokea nchini India.

Kwa mujibu wa mtandao wa indiacurents neno biriani lina asili ya kiajemi (sasa hivi Iran) lkimaanisha “kaangwa kabla ya kupika”.

Huenda asili ya jina hili ikatuambia mengi zaidi juu ya wapi pishi hili limetokea, hebu tuachane na asili ya pishi hili, leo tusogee jikoni na kuandaa biriani itakayoliwa na rosti ya nyama ya ng’ombe.

Maandalizi

Osha nyama ikate vipande vya saizi na uichemshe mpaka iive. Wakati unasubiri nyama iive, chambua mchele wa basmati na uuloweke kwa muda wa saa mbili.

Menya viazi kisha osha pamoja na karoti, hoho na vitunguu na ukate kwa saizi unayotaka.

Washa jiko, bandika sufuria yenye mafuta kiasi kaanga vitunguu kwa dakika tano mpaka viwe vya kahawia, vitoe kisha kaanga viazi kwenye mafuta hayo hayo uliyokaangia vitunguu. 

Weka nyama kwenye sufuria lingine, ongeza mafuta kidogo na karoti ya kusaga kisha ukoroge mpaka vichanganyike vizuri, ongeza nyanya  funika kwa dakika 5 mpaka iive.

Ongeza supu ya nyama, hoho, viazi na vitunguu ulivyokaanga mwanzoni.

Wakati rosti likiendelea kuchemka ongeza ladha ya chokoleti au vanila. Wengine hupendelea mtindi, kisha acha ichemke kidogo tu.

Sasa rosti lako lipo tayari, tuelekee kwenye kupika biriani.

Baada ya kuloweka mchele kwa saa mbili, andaa jiko chemsha maji utakayoyatumia kupika biriani yako.

Weka iriki, binzari nyembamba na mdalasini au vijiko viwili vya pilau mix, chumvi na uache biriani yako ichemke kwa dakika 20.

Biriani ikichemka epua na umwage maji yote yaliyobakia uhakikishe biriani yako imebaki kavu.

Baada ya hapo weka sufuria yenye mafuta jikoni. Yakichemka, kaanga biriani yako kisha weka moto mdogo ufunike iive.

Biriani yako ikiwa inaendelea kuiva koronga rangi ya chakula (food colour) kijiko kimoja kidogo cha chakula na vijiko vitano vya maji kwenye glasi kisha unyunyizie biriani yako ili kuipa rangi.

Unaweza kutumia rangi zaidi ya moja kama unapenda, ukimaliza funika biriani iive vizuri.

Ukihakikisha biriani yako imeiva vizuri, ongeza vitunguu vilivyokaangwa, changanya vizuri.

Mpaka hapo biriani yako ipo tayari kuliwa pamoja na rojo (roast) iliyoandaliwa mwanzoni.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa