Unavyoweza kupika kalmati laini nyumbani

Na Fatuma Hussein
28 Mar 2024
Tujifunze mapishi ya kalmati zinazoweza kuwa miongoni mwa vitafunwa  katika msimu huu au wakati mwingine wowote utakaopendea
article
  • Utahitaji unga wa ngano, hamira, chumvi, sukari, hamira na maji ili kuandaa
  • Ikiwa hutumii sukari au mafuta mengi kwenye chakula basi kitafunwa hiki hakitakufaa 

Umeshawahi kula kalmati? Bila shaka unafahamu utamu wake na jinsi zinavyoweza kuvutia walaji.

Sasa kabla kipindi cha mfungo hakijaisha tujifunze mapishi ya kalmati zinazoweza kuwa miongoni mwa vitafunwa  katika msimu huu au wakati mwingine wowote utakaopendelea.

Ikiwa hutumii sukari au mafuta mengi kwenye chakula basi kitafunwa hiki hakitakufaa kutokana na kuhitaji sukari nyingi wakati wa  maandalizi.

Tuingie jikoni

Maandazi ya kitafuwa hiki huanza kwa kuandaa unga wa ngano ambapo utauweka kwenye bakuli au chombo kisafi ili  kuondoa uchafu kama ukiwepo kisha uendelee kwa kuongeza hamira, siagi au mafuta ya kupikia,sukari, chumvi  na maji kiasi.

Baada ya hapo anza kuchanganya unga taratibu huku ukiongeza maji mpaka pale unga utakapolainika. Katika hatua hii utachanganya unga kama vile inavyofanyika katika kuandaa chapati za maji.

Hakikisha umechanganya hadi pale utakakpopata mchanganyiko mzito kisha uache uumuke kwa dakika 15.

Ukishaumuka bandika mafuta jikoni na yakipata moto uanze kuchota unga wako kidogo kidogo kwa kutumia mkono au kijiko na kuweka katika karai la mafuta.

Shira huvifaya vitafunwa hivi kuvutia na kuwa na muonekano mzuri kwa nje.Picha|Raihanna Cuisine

Katika hatua hii wapo wanaotumia chupa ili kukata maumbo ya kalmati na wengine hukunja mfuko laini kwa umbo la koni kisha kutoboa mbele ili kurahisha hatua ya kuchoma kalmati.

Choma kalmatimpaka pale zitakapokuwa na rangi ya kahawia uziepue zichuje mafuta kisha uzitandaze katika sahani au sinia tayari kwa kuzimiminia shira (sukari ya kupika).

Shira ndiyo huzipa kalmati muonekano mzuri kwa nje.Ikiwa hufahamu jinsi ya kutengeneza shira, usijali  fuatilia makala ijayo.

Baada ya hatua hiyo kalmati zako zitkuwa tayari kwa kuliwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa