Unavyoweza kupika rosti ya maini na kabichi

Na Lucy Samson
16 Mar 2023
Mboga hii ni bana bajeti kwa wale wenye familia kubwa yenye watu sita au zaidi.
article
  • Mboga hii inafaa kwa wenye familia kubwa wanaotaka kubana bajeti
  • Unaweza kuandaa pishi hili kwa muda mfupi

Maini ni moja ya mboga inayopendwa na wengi kutokana na ladha yake pamoja na urahisi wa kuipika ukilinganisha na mboga nyingine.

Si hayo tu mboga hii hunogesha vyema kitafunwa cha asubuhi na kukuachia ladha tamu itakayofanya asubuhi yako kwenda vizuri.

Katika kuendeleza ubunifu kwenye masuala mazima ya mapishi leo tuandae mchanganyiko wa maini na kabichi, rosti tamu unalowezakupika kw kwa jiko la gesi au umeme. 

Mboga hii pia ni bana bajeti. Kama ulikuwa unahitaji maini kilo moja kwa ajili ya mahitaji ya familia ya watu sita, kupitia pishi hili unaweza kununua maini nusu kilo na kabichi moja tu na ikatosha.

Kwa mama ntilie na wauza migahawa pia wanaweza kujaribu kuandaa pishi hili na kuongeza ladha na virutubisho zaidi kwa wateja wao.

Vuta jiko tuandae mboga yetu

Huku hatuna maandalizi mengi ni kuosha maini na kuyakatakata, kuosha kabichi na kulikatakata na kuandaa nyanya, kitunguu, karoti, pamoja na hoho.

Menya kitunguu swaumu na tangawizi kisha saga kwenye blenda au twanga mpaka vilainike.

Baada ya hapo washa jiko, chemsha maini pamoja na kitunguu swaumu kilichosagwa, tangawizi pamoja na chumvi mpaka yaive.

Maini yakiiva bandika sufuria nyingine jikoni weka mafuta kiasi anza kuweka vitunguu, karoti na hoho kisha ukaange mpaka viive.

Vikiiva ongeza nyanya na nyanya ya pakti acha zichemke kwa dakika 5 kisha ongeza kabichi na ufunike ziive.

Baada ya kuridhishwa na kiwango cha uivaji wa kabichi yako ongeza maini uliyoyachemsha, ongeza chumvi  kiasi na ukoroge ichanganyike vizuri na kabichi.

Ongeza Garam masala, na curry poda (viungo vya mchuzi) au viungo vyovyote vya mchuzi unavyopendelea kisha uache mboga iive kwa dakika nyinginee tano na mboga yako itakuwa tayari.

Unaweza kula mboga hii na ugali, wali, ndizi za kukaanga, mihogo chapati ama kitafunwa kingine chochote.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa