Je, unatumia nishati gani ya kupikia ndizi nyama nyumbani kwako?
Kumekuwa na mitazamo tofauti ya kupika chakula kwenye umeme, wapo wanaosema kinapoteza radha na wapo wanaodai umeme unatumika mwingi.
Wapo wanaoogopa kuwa linaweza kusababisha shoti, hivyo kulazimika kutumia aina nyingine za nishati.
Pamoja na mitazamo yote hiyo, leo tutatumia dakika 35 kuandaa chakula chetu cha ndizi nyama na kitakuwa tayari kwa kuliwa.
Twende jikoni
Osha nyama kisha katakata kulingana na vipande vya ukubwa unaopendelea, changanya nyama, chumvi na tangawizi iliyopondwa. Ongeza vikombe viwili vya maji kisha bandika kwenye sufuria maalum la kupikia kwenye jiko la umeme na uache kwa muda wa dakika 20.
Wakati nyama ikiiva, paka mikono yako mafuta kidogo ya kupikia kisha menya ndizi na viazi, vikate na uviweke kwenye sufuria yenye maji safi. Baadaye andaa mahitaji mengine kama kitunguu, karoti na pilipili hoho.
Ukipika nyama, subiri presha iishe kisha fungua mfuniko wa sufuria yako kisha changanya ndizi, viazi, viungo vyote na mafuta. Funika tena na pika kwa muda wa dakika 10.
Muda wa kupika ukiisha ondoa presha kisha weka tui na acha ichemke kwa muda wa dakika 5 jiko likiwa wazi. Chakula kitakuwa tayari na kipeleke mezani ukafurahie wewe na uwapendao.