Vyakula rafiki kwa wagonjwa wa figo

Na Esau Ng'umbi
7 Jun 2022
Ni pamoja na protini nyepesi na nafaka zisizokobolewa. Mboga za majani na matunda. Ugonjwa wa figo ni moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo pamoja na sababu nyingine yanayohusiana pia na ulaji usiofaa na mtindo ya maisha. Kitabu cha lishe na  ulaji unaofaa kwa  watu wenye magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza cha mwaka 2014 kilichotolewa […]
article

  • Ni pamoja na protini nyepesi na nafaka zisizokobolewa.
  • Mboga za majani na matunda.

Ugonjwa wa figo ni moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo pamoja na sababu nyingine yanayohusiana pia na ulaji usiofaa na mtindo ya maisha.

Kitabu cha lishe na  ulaji unaofaa kwa  watu wenye magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza cha mwaka 2014 kilichotolewa na Wizara ya Afya na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA) pamoja na Shirika la Kisukari Duniani (WDF) cha kinaeleza kuwa mgonjwa wa figo anatakiwa kuwa makini katika ulaji wa chakula.

Anatakiwa kudhibiti ulaji wake kwa kufanya mabadiliko ya aidha kupunguza kiasi au kuacha kula aina fulani ya vyakula. 

Pamoja na ukweli kuwa kila mgonjwa hupewa ushauri wa ulaji kulingana na hali na matakwa yake kuna baadhi ya ushauri ambao unawahusu wagonjwa wote.

Vyakula hivi vinaweza kutumiwa na wagonjwa wa figo ili kuwawezesha kuimarika kila siku: 

Kabeji iliyopikwa

Kabeji ni miongoni mwa mbogamboga ambazo hazina madini ya potasiamu kwa kiasi kikubwa ambayo ni hatari kwa mtu mwenye ugonjwa wa figo.

Katika kundi la mbogamboga, mgonjwa wa figo anashauriwa kula kabeji kwa wingi. Vyakula vingine vyenye kiasi kidogo cha potasiamu ni pamoja na maharage machanga (green beans), karoti iliyopikwa, mahindi mabichi, tango, bilinganya, letusi, mbata, kitunguu, giligilani, njegere, pilipili mbichi na spinachi mbichi.

Dk Juma Kilaghai kutoka taasisi ya afya ya Herbal Impact anasema mwili wa mgonjwa wa figo haupaswi kupata vyakula vyenye madini ya potasiamu kwa wingi kama parachichi, ndizi, nazi, embe, chungwa, peasi, komamanga, tende, viazi vikuu, viazi vitamu, viazi ulaya, na matunda yaliyokaushwa.

“Ni rahisi sana kwa mgonjwa wa figo kulundika kiasi kikubwa cha potasiumu mwilini kwa kuwa kiasi cha madini hayo kinachoondoka mwilini kwa njia ya mkojo ni kidogo sana. 

“Hii ina maana kuwa, watu wenye maradhi ya figo wanatakiwa kuwa makini sana na kiasi cha madini ya potasiumu kinachongia mwilini mwao,” amesema Dk  Kilaghai.

Mboga hiyo itamsaidia mtu mwenye matatizo ya figo kwa sababu ina madini machache ya potasiumu. Picha| Unsplash.

Wali mweupe

Chakula hicho kinashauriwa kutumiwa na watu wenye tatizo la figo kwa sababu mwili hatumii nguvu kubwa kukimeng’enya. Nafaka nyingine zinazoweza kutumiwa ni shayiri, ngano na mahindi lakini kwa kiasi kidogo.

Tunda la tufaha

Dk Kilaghai anabainisha kuwa tunda la tufaha (apple), ni miongoni mwa matunda ambayo mgonjwa wa figo anaweza kutumia kila siku katika mlo wake kutokana na kuwa na virutubisho ambavyo huisaidia figo kuondoa asidi.

Matunda mengine ni pamoja na matunda ya jamii ya zambarau, zabibu, balungi, nanasi, tikiti, na “strawberries”.

Vyakula vyenye protini nyepesi

Kitabu cha lishe na ulaji unaofaa kinabainisha kuwa ni muhimu kuepuka vyakula venye protini nyingi kwani metaboli ya protini huzidisha mabaki kama vile urea, amonia na “creatinine” ambayo tayari yako juu kwa mtu mwenye ugonjwa wa figo na huleta madhara mwilini. 

Inashauriwa kula protini ambazo zinatumiwa na mwili kwa ufanisi bila kuacha mabaki mengi. Vyakula vyenye protini hizo ni pamoja na mayai, samaki, nyama ya kuku, maziwa na jibini.

Vyakula vyenye kalori

Kwa mujibu wa Taasisi ya kimataifa ya Elimu ya Figo inabainisha kuwa mwili huhitaji kalori kwa shughuli za kila siku na pia kudumisha halijoto, ukuaji na uzito wa kutosha wa mwili. 

Kalori hupatikana hasa kwenye kabohaidreti na mafuta na mahitaji ya kalori kwa wagonjwa wa figo ni 35-40 kcals/kg kwa uzito wa mwili kwa siku.

Kalori hupatikana kwenye vyakula vya  kabohaidreti kama ngano (mkate), nafaka, mchele, viazi, ingawa wanashauriwa kutumia nafaka zisizokobolewa.

Vyakula vyenye nyuzi nyuzi na visivyokobolewa husaidia kurahisisha mmeng’enyo wa chakula mwili. Picha| Unsplash

Kinachosababisha tatizo la figo

Dk Kilaghai anaeleza kuwa maradhi ya figo husababishwa na mrundikano wa asidi mwilini ambayo hutokana na vyakula tunavyokula kila siku ambavyo vikishameng’enywa na kufyonzwa virutubisho mabaki yake hutolewa kwa njia ya taka mwili kama jasho au mkojo.

Figo huchuja taka hizo, hivyo kutokana na kuwepo kwa asidi nyingi kwenye taka hizo figo huathirika polepole na mpaka kufeli kabisa.

Anashauri watu kupunguza matumizi ya vyakula vyenye protini na wanga kupita kiasi na kutumia matunda kwa wingi ambayo husaidia kupunguza kiwango cha asidi mwilini.

“Watu wengi wanaathirika figo kwa sababu wamefocus zaidi kwenye diet ya protini na wanga na vile vyakula vinavyowapa ulinzi wanavitumia kwa kiwango kidogo sana.

“Vyakula vinavyowapa ulinzi ni vyakula vyenye madini ya alkali kama sodiam, potasiamu, magnesiamu, calsiamu na lisiamu. Haya madini yanapatikana kwenye vyakula vya mboga mboga na matunda…..kwa hiyo kwa sababu hatuli vyakula hivi kwa wingi hivyo hivyo ile asidi  haitapoozwa na kuzidi kuongezeka mwishowe kuathiri figo,” anasema Dk Kilaghai.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa