Vyakula rahisi vya kujifunza mabachela mwaka 2022

Na Mwandishi Wetu
4 Jan 2022
Unaweza kula nyama na ugali mchana, na hata usiku.
article

  • Nyama ya mchuzi inahitaji viungo vichache
  • Ugali unahitaji nguvu zako na hesabu za makadirio ili kuupika ipasavyo
  • Mchicha kupika ni kama kunywa maji tu. 

Kupika siyo kazi ngumu kama unavyodhani. Jambo la muhimu hapa ni kujua viungo unavyohitaji kwa ajili ya kutengeneza pishi fulani unalotaka wewe na familia yako mfurahie. 

Katika upishi pia, siyo lazima kuanza kwa kupika vyakula vinavyohitaji mambo mengi. Vipo baadhi ya vyakula vinavyohitaji viungo vitatu tu, pengine hata viwili au kimoja na ukapata mlo wa maana na wenye virutubisho vyote. 

Haya ni baadhi ya mapendekezo ya vyakula kutoka kwa timu ya Jiko Point kwa mabachela wanaoanza kupika:-

Nyama ya mchuzi

Hii ni moja ya mboga mashuhuri. Wengi tumekuwa tukiila hii. Kuipika mboga hii, unachohitaji hapa ni nyama, kitunguu, nyanya, karoti na hoho. 

Kiwango cha nyama kinategemea na mfuko wako na uwezo wa kuhifadhi yaani kama una jokofu ama la.  Robo kilo ya nyama kwa bachela mmoja freshi tu. 

Viungo vingine ni mafuta, jiko la kupikia na sufuria pamoja na mwiko.

Nyama inaweza kufurahiwa na vyakula vingine kama wali, pilau, ndizi na chapati. Picha| Delachieve.

Chemsha nyama kwa dakika 30, onja na ukiona imelainika kama unavyotaka, ni muda wa kuandaa mchuzi. 

Mimina mafuta kidogo kwenye sufuria, kisha kaanga kitunguu, ongezea karoti na kisha weka nyanya zilizokatwa vipande vidogo vidogo. Hiyo itasaidia viive na kulainika haraka kupata mchuzi.

Funika viache viive walau kwa dakika tano hivi, maji yakikauka weka nyama iliyokwisha iva na kisha changanya kwa muda. 

Ongeza vikorombwezo vingine kama beef masala, pilipili manga au pilipili hoho. Hapo ushamaliza mzee baba.

Ugali wa sembe

Kila mtu ana njia zake za mapishi ya ugali. Hata hapa tutumia njia ambayo ni maarufu kwa wengi.  

Weka unga wa sembe kwenye bakuli na kisha changanya kupata kimiminika. Weka maji jikoni na subiri yachemke. 

Yakishachemka, weka kimiminika cha unga huku ukikoroga, kama unatengeneza uji. Kisha koroga hadi uji wako uanze kutokota. 

Acha utokote kama dakika tano hivi kisha anza kuweka unga mdogo mdogo.

Songa ugali wako ukitumia nguvu na kuhakikisha hakuna bonge la unga linalobaki bila kusongwa. Hesabu kubwa hapa ni za makadirio ya unga na maji uliyoweka ili usije kuwa na ugali mgumu sana.

Unaweza kula ugali na nyama yako ya mchuzi na maisha yakaendelea. 

Ugali unapanda na mboga mbali mbali ikiwemo samaki, nyama kavu, kisamvu, mlenda na kuku. Picha| Radio Jambo.

Namna ya kupika Mchicha

Hili pishi ni moja ya mapishi rahisi kabisa ambayo unaweza kuyafanya ndani ya dakika chache tu. Ni kama kunywa maji. Unatakiwa kuchambua mchicha wako na kisha kuuosha vizuri kuhakikisha hauna mchanga unaoweza kuwakwaza walaji. 

Hatua inayofuata ni kukaanga vitunguu na kisha kuweka mchicha wako kwenye sufuria inayokaanga vitunguu.

Geuza mchicha huo kwa kama dakika tatu hivi na ukishaona umenyauka, weka chumvi na kisha endelea kugeuza. 

Wengine huongeza hoho, karoti, lakini hayo ni maamuzi tu.

Kwa haraka, kama una jiko na masufuria, utakuwa unahitaji mafuta ya kupikia, nyanya, hoho, vitunguu, nyama, karoti, mchicha na unga. Gharama yake kwa mlo wa mtu mmoja, inaweza isizidi hata Sh 5,000.

Kazi kwako sasa. Unakisingizio gani cha kutokupika mwaka 2022? 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa