Dar es Salaam. Ni matamanio ya kila mzazi na mlezi kuhakikisha mtoto wake anakuwa na uelewa mzuri wa kimasomo na kumbukumbu nzuri itakayomuwezesha kufanya vizuri kwenye mitihani na masuala mengine katika maisha .
Licha ya uwepo wa matamanio hayo, ni watoto au vijana wachache wanaofanikiwa kufanya vizuri kwenye masomo huku wengine wakiishia kufeli.
Hivi karibuni Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) Athuman Amasi, alitangaza matokeo ya kidato cha pili na darasa la nne huku ufaulu ukishuka kwa asilimia 3.4 kwa darasa la nne na asilimia 7.4 kwa kidato cha pili.
Baadhi ya wataalamu wa afya wanaeleza kuwa watoto wenye matatizo ya lishe ikiwemo utapiamlo hushindwa kufanya vema darasani ukilinganisha na wale wanaopata mlo kamili wenye virutubisho vyote.
Huenda kushuka kwa ufaulu huu kunasababishwa na uelewa na kumbukumbu ndogo ya kimasomo iliyowafanya baadhi yao kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani hiyo ya kitaifa.
Chakula tunachotumia kila siku kina mchango mkubwa katika uimarishaji wa afya ya ubongo na kumbukumbu.
“Vyakula unavyokula vina jukumu la kuweka ubongo wako ukiwa na afya na vinaweza kuboresha kazi maalum zinazofanya na ubongo kama vile kuimarisha kumbukumbu na umakini,” inasema tovuti ya Healthline.
Ili kuimarisha ubongo wako baadhi ya wataalamu wa afya wanasema kuwa aina au makundi yote ya vyakula yana umuhimu kwa mtoto anayekua ili kuimarisha mfumo wa kinga mwili na mfumo wa kumbukumbu.
Daktari wa masuala ya lishe, kutoka Kliniki ya tiba asili ya Conwell Naturopathic iliyopo jijini Dar es Salaam, Dk Elizabeth Lema anasema mfumo wa mwili wa mtoto ukiwa na virutubisho sahihi utamuwezesha mtoto kuelewa masomo na siyo kukariri.
Ikiwa unatamani kuimarisha kumbukumbu na uelewa wa mtoto wako darasani usihofu, makala hii imeainisha makundi ya vyakula vitakavyoimarisha afya ya mtoto wako.
Vyakula vya ziwani, baharini
Aina nyingi ya vyakula vinavyopatikana baharini au ziwani vina wingi wa madini ya chuma, Omega 3, 6 na 9 ambayo yanahusika kwa kiasi kikubwa kuimarisha afya ya akili na kumbukumbu.
Vyakula hiyo ni pamoja na aina zote za samaki zinazopatikana ziwani na baharini ikiwemo Sato, Sangara, Migebuka, Kibua, Kolekole na Mkunga.
Kupitia vyakula vya baharini pia unaweza ukapata mafuta na unga wa samaki wenye faida nyingi mwilini.
Dk Elizabeth anasema mafuta yanayozalishwa na samaki hao huchochea mfumo wa fahamu na kuongeza uwezo wa kufikiri.
“Nashauri wazazi wawape watoto mafuta ya samaki kwa sababu yanasaidia sana kuimarisha ukuaji na uwezo wao wa kufocus (uzingativu) kwenye masomo,” ameongeza Dk Elizabeth.
Mbali na faida hizo tovuti ya masuala ya afya Healthline inasema vyakula vya baharini au ziwani husaidia mfumo wa moyo kufanya kazi vema na ni chanzo cha madini chuma na vitamini mbalimbali ikiwemo vitamini D.
Vyakula vya mbegu za nafaka
Kundi hili la chakula linahusisha karanga, mbegu za maboga, alizeti na uwele.
Kundi hili la chakula husaidia upatikanaji wa mafuta lishe yenye faida nyingi kwenye maendeleo ya ukuaji wa akili ya mtoto pamoja na kuimarisha kumbukumbu.
“Zamani tulikuwa tunashauri watoto wapewe mafuta ya samaki lakini kwa sasa ukipata mafuta ya mbegu inaweza kuwa bora zaidi kuliko mafuta ya samaki,” anasema Dk Elizabeth.
Aina nyingi ya mbegu hizi pia zimebeba aina nyingine ya madini ikiwemo Madini ya chuma, zinki, pamoja na kopa inayohusika kudhibiti mfumo wa neva.
Vyakula vya mizizi
Vyakula hivi ni pamoja na viazi vitamu, mihogo, viazi vikuu, viazi vitamu, muhogo, magimbi, viazi mviringo na ndizi za kupika.
Vyakula hivi vina nyuzi nyuzi zinazosaidia mfumo wa mmengenyo wa chakula ambao Dk Elizabeth anasema unahusika moja kwa moja na mfumo mzima wa ubongo.
“Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa mtoto usipokuwa vizuri akili yake haifanyi kazi vizuri kwa sababu tumbo ni kama aina nyingine ya mfumo wa akili,” ameongeza Dk Lema.
Mboga mboga na matunda
Kundi hili linasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kuzalisha vitamini C inayohitajika mwilini kuimarisha mfumo wa kinga mwili pamoja na kuimarisha mfumo wa moyo na mishipa kwa mujibu wa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Marekani (NIH).
Mbali na vitamini hivyo mboga mboga kama maboga na mboga za majani hulinda mwili dhidi ya maradhi pamoja na kusaidia mwili kufanya kazi zake vizuri ikiwemo mfumo wa afya ya akili na kuboresha kumbukumbumbu.
Mazoezi hufanya akili kuwa moto
Mbali na vyakula hivyo, Dk Lema ameshauri vitu vingine vinavyoweza kuboresha afya ya akili ikiwemo kufanya mazoezi na kupata muda wa kupumzika kwa saa nane.
Ikiwa mtoto wako amedumaa kimwili au unaona dalili za kudumaa kiakili daktari huyo ameshauri ufuatiliaji wa karibu wa lishe kama ilivyoainishwa hapo juu pamoja na msaada wa kisaikolojia ili hali yake irudi kama watoto wengine.