Ni ukweli ulio bayana kuwa, miongoni mwa misingi ya afya bora ni pamoja na kula chakula, baadhi ya vyakula vina virutubisho muhimu ambayo husaidia kuimarisha afya zetu katika maeneo mbalimbali mwilini ikiwemo kuboresha uoni.
Mtindo wa maisha hivi sasa umewafanya watu wengi kupata changamoto ya uoni, baadhi wakishindwa kuona kabisa huku wengine wakipata changamoto ya kuona karibu au mbali.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Watanzania 620,000 wanakabiliwa na matatizo ya kutoona wakati milioni 1.86 wakiwa na chagamoto ya kuona kwa viwango vya kati na juu.
Hata hivyo, pamoja na matibabu yanayotolewa kwenye vituo vya afya ubora wa lishe ni muhimu kwa ajili ya kudumisha uwezo wa macho kuona vyema.
Vyakula vyenye virutubisho kama vile ‘lutein, zeaxanthin, omega-3 fatty acids, na vitamini A na E’ akwa kiasi kikubwa vinasaidia kulinda afya ya macho dhidi ya athari zinazohusiana na umri, asili ya kazi au matatizo ya kurithi.
Makala hii inaangazia baadhi ya vyakula muhimu ambavyo vinasaidia kuboresha uoni, ambapo Nukta Habari imerejea machapisho ya tafiti za kisayansi pamoja na kuzungumza na wataalamu wa lishe.
Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya vyakula mahususi kwa ajili ya kuboresha afya ya macho
Mboga mboga
Tafiti za afya zinaonesha kuwa ulaji wa mboga mboga kama brocoli, spinachi, mchicha, majani ya maboga, kisamvu, majani ya kunde, matembele, mnafu na mchunga unaweza kusaidia kuimarisha afya ya macho.
Utafiti uliofanywa na taasisi ya macho ya American Optometric Association ya Marekani umebaini mmea huu kuwa na kirutubisho cha ‘indole-3-carbino’ inayosaidia kuondoa sumu kwenye retina, na kupunguza hatari kwa watu wazima kupoteza uwezo wa kuona kunakosababishwa na kupungua kwa nguvu ya seli za macho.
Brokoli pia ina virutubisho vvya lutein na zeaxanthin, ambavyo hulinda macho dhidi ya miale ya mwanga yenye nguvu kama mionzi ya jua, pia ina pigmenti lishe za pekee ambazo hupatikana kwenye retina, hasa sehemu iitwayo ‘macula’ iliyopo nyuma ya jicho.
Samaki
Samaki wana kiwango kikubwa cha madini ya ‘omega-3 fatty acids’ ambayo ni muhimu kwa ajili ya kudumisha afya ya retina iliyopo nyuma ya jicho, pia huepusha macho kuwa makavu na kuzorota kwa seli.
Samaki kama kaa ni miongoni mwa vyanzo vizuri vya madini ya zinki, ambayo hutumika kama chombo cha kusafirisha vitamini A kutoka kwenye ini hadi kwenye retina na kulinda macho dhidi ya athari mbaya za mwanga mkali wa jua.
Karoti
Zao hili limezoeleka na wengi kama miongoni mwa tiba bora za macho, hii ni kwa sababu karoti ina madini mengi sana ya “beta-carotene”, virutubisho ambavyo mwili huvitumia kutengeneza vitamini A ambavyo husaidia kuona kwenye mwanga hafifu na kutoona kwa karibu.
Pia karoti ina ‘ontioxidant’ ya lutein inayosaidia kupunguza hatari ya kusumbuliwa na macho kadri umri unavyokwenda.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) upungufu wa vitamini A huchangia takribani watoto nusu milioni kuwa vipofu kila mwaka
Mbegu za alizeti
Mbegu hizi zina vitamini E kwa wingi ambayo ni muhimu kuepusha kuzorota kwa seli za macho kadri umri unavyozidi kuongezeka, aidha, mbegu hizo zimejaa protini na mafuta muhimu ambayo husaidia kupunguza uvimbe na kuondoa taka za kimetaboliki kwenye macho.
Kiwi
Tunda hili lina madini muhimu ya ‘zeaxanthin’ na ‘lutein’ ambazo husaidia kupunguza ukali wa mwanga wa jua au kutoka kwenye vyanzo visivyo vya asili ambavyo vinaweza kuharibu sehemu muhimu ya jicho yaani retina.
Pia husaidia kulinda dhidi ya mtoto wa jicho na kuzorota kwa seli kunakotokana na umri kuongezeka.
Machungwa pamoja na machenza ni miongoni mwa matunda yanayopendekezwa na wataalamu wa afya kwa kuwa yana wingi wa vitamini C ambayo ni muhimu kwa uimara wa macho.
Vyakula vyenye asili ya protini.
Ukitaka kuboresha uoni wako hakikisha hukosi kula vyakula vyenye utajiri wa protini asilia kama mayai kwa kuwa yana muunganiko wa virutubisho vyote ambavyo jicho linahitaji kuwa na afya bora kwani kiini cha yai kina vitamini A, ‘lutein, zeaxanthin’ na zinki. Vitamini A hulinda sehemu ya mbele ya jicho iitwayo konea.
Utafiti uliofanywa nchini Scotland mwaka 2019 ulihitimisha kuwa kula mayai kwa wastani wa mayai mawili hadi manne kwa wiki hupunguza hatari ya kudhoofu kwa mishipa ya macho.
Aidha, virutubisho vilivyopo kwenye maziwa hutajwa kama chanzo kizuri cha ‘riboflavin’ yaani vitamini B2 ambayo sio tu husaidia kuepusha hatari ya ugonjwa wa mtoto wa jicho, bali pia afya ya ngozi, mfumo wa umeng’enyaji chakula, seli za damu na kazi za ubongo.
Chanzo kingine kizuri cha protini ni lozi, hili ni zao linalofanana na karanga ambalo lina wingi wa vitamini E inayosaidia kulinda tishu zilizo kwenye macho, pia huepusha kuzorota kwa sehemu ya jicho iliyo katikati ya retina pamoja na mtoto wa jicho.
Viazi vitamu
Kama ilivyo karoti, viazi vitamu vina virutubisho muhimu vya vitamini A na beta-carotene vinavyosaidia kuona vyema. Vinaepusha maambukizi ya bakteria na virusi vinavyoshambulia macho kwa kuimarisha sehemu ya juu ya jicho na utando wa utelezi.
Pia husaidia kuzuia mtoto wa jicho, glakoma, kuzorota kwa misuli ya jicho na kuepusha macho kuwa makavu.
Mwandishi wa habar wa kujitegemea Rodgers George, ameiambia Nukta Habari kuwa matumizi ya mara kwa mara ya vifaa vya kielektroniki vilisababisha kupata changamoto ya macho ambapo alishauriwa na matabibu kutumia zaidi vyakula vyenye lishe ya macho.
“Daktari wa macho alinishauri kula mboga za majani hususan za kijani kibichi, samaki, sharubati ya karoti, matunda na viazi vitamu…baada ya takribani mwaka mmoja nilipata ahueni na kuacha kuvaa miwani,” amesema Rodgers.
Ikumbukwe kuwa kwa kadri muda unavyozidi kwenda miili yetu inapungua nguvu na uwezo wa kupambana na magonjwa, wazee wanashauriwa kuzingatia ulaji wa vyakula vyenye virutubisho vingi kama matunda na mbogamboga kwa kuwa husaidia kuzalisha kinga ya magonjwa.
Mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe nchini (TFNC) Devota Mushumbusi, ameiambia Nukta Habari kuwa, ni vyema kuweka utaratibu wa kula vyakula vyenye vitamini mara kwa mara kwa kuwa vinapatikana kwa urahisi na hufanya kazi muhimu mwilini.
“Vitamini A ambayo kwa wingi hupatikana kwenye mboga mboga na matunda inasaidia kuimarisha macho, kuona vyema hususan wakati wa usiku na mazingira yenye mwanga hafifu, kwa sababu inatoa pigmenti zinazosaidia macho kuona na kuzalisha uteute kuepusha jicho kukwaruzika,” amebainisha Mushumbusi.
Mushumbusi ametoa rai kwa wazazi wenye watoto wadogo kuwapa kuwapa mchanganyiko wenye mbogamboga, samaki, maboga, ili kuwaepusha na matatizo ya macho yanayoweza kuwaanza mapema kwenye hatua za awali za ukuaji.