Vyakula vya kumlisha mtoto baada ya miezi sita

Na Mwandishi Wetu
9 May 2022
Wataalamu wa afya wanashauri kuwa mama anatakiwa kumnyonyesha mtoto hadi miaka miwili na zaidi hata baada ya kuanza kula chakula.
article
  • Anza kwa kumpa vyakula laini na kuendelea kuboresha lishe yake kadri anavyozidi kukua.
  • Usiache kumnyonyesha maziwa ya mama hadi atakapotimiza miaka miwili au zaidi.

Kila siku wazazi wapya huanza safari ya malezi ya watoto wao wachanga. Wazazi hawa pamoja na kupata elimu ya kliniki namna ya kuwalisha watoto wao, baadhi hujikuta njia panda ya aina ya vyakula vya kuwalisha baada ya kutimiza miezi sita.

Ikumbukwe kuwa miezi sita ya awali baada ya kuzaliwa mtoto anatakiwa kunyonya maziwa mama pekee bila kuchanganyiwa chakula chochote kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya. 

Hata hivyo, baada ya miezi sita mtoto hutakiwa kuanza kulishwa chakula taratibu kwa kuwa maziwa ya mama pekee hayawezi kumtosheleza mtoto. Hii haimaanishi kuwa mama ataacha kumnyonyesha mtoto, la hasha. Mama atatakiwa kumnyonyesha mtoto mpaka atakapotimiza miaka miwili au zaidi. 

Taasisi ya Lishe na Chakula Tanzania (TFNC) inaeleza kuwa baada kutimiza miezi sita mtoto anahitaji kulishwa taratibu vyakula mchanganyiko na vya kutosha ili akue vizuri. Utatakiwa kumnyonyesha mtoto na kumlisha hadi atapafika zaidi ya miaka miwili kabla hujaanza mipango yako ya kumpata mwingine. 

Hatua muhimu mtoto anapoanza kula hadi atakapofika miaka miwili 

Anza na chakula laini

TFNC inashauri kuwa unapaswa kumpatia mtoto kijiko kimoja au viwili vya chakula laini mara mbili kwa siku. Kadri siku zinavyoenda utatakiwa kuongeza taratibu kiasi, uzito na aina ya vyakula kutokana na kasi ya ukuaji wa mtoto. 

Ila ni muhimu mara anapotimiza umri wa miezi sita chakula cha kuanzia kinapaswa kuwa laini ila kisiwe chapesi au majimaji sana. Uji ni moja ya vyakula muhimu vya awali. 

 Mtoto akianza kuzoea kula

Baada ya mtoto kuanza kuzoea kula na kutafuna aina mbalimbali ulivyomuanzishia, taasisi hiyo ya Serikali inayosimamia lishe inashauri uanze kumlisha mtoto vyakula livyopondwapondwa na vizito zaidi tofauti na laini vya awali. 

Vyakula muhimu vya kuboresha mlo wa mtoto

Kwa mujibu wa TFNC mzazi anapaswa kuendelea kuboresha chakula cha mtoto kama uji na vyakula vingine kwa kuweka maziwa, karanga zilizokaangwa na kupondwapondwa na mbegu nyingine za mafuta ambazo zinafaa kuchanganywa. 

Usisahau vyakula jamii ya kunde

Ni dhahiri utakuwa unampa mtoto wako vyakula vikuu kama wali, uji, vizi na ndizi za kuponda lakini wataalamu wa lishe wanashauri umpatie mtoto vyakula jamii ya kunde, nyama, kuku, samaki, mboga ya majani na matunda kila siku. Vyakula hivi ni muhimu kwa mtoto kwa kuwa humpatia virutubishi. 

Vipi kuhusu sukari na mafuta? 

Iwapo ulikuwa unajiuliza kama unatakiwa kuweka mafuta na sukari kwenye chakula cha mtoto, ndiyo hujakosea. Wataalamu wa lishe wanashauri kuwa unaweza kuongeza sukari na mafuta kwenye chakula cha mtoto ila kwa kiasi ili kumuongezea nishati na lishe. 

TFNC inasema kuwa mafuta husaidia ufyonzaji wa haraka wa baadhi ya vitamini na huongeza ladha kwenye chakula ambacho watoto hufurahia. 

Tumia unga wa kimea kurahisisha mmeng’enyo wa chakula

Chakula cha mtoto kina mahitaji mengi  na baadhi ya masuala mengine unayopaswa kuzingatia kwa mujibu wa TFNC ni kutumia unga wa kimea na vyakula vilivyochachushwa ili kuongeza ubora na uyeyushaji wa chakula tumboni kwa mtoto. 

Pamoja na mbinu zote hizo wakati wote hakikisha chakula cha mtoto kinaandaliwa katika mazingira safi na salama. Watoto ni rahisi kupata magonjwa hivyo nawa mikono yako kwa sabuni na maji tiririka kabla ya kutayarisha chakula, kabla na baada ya kumlisha mtoto na utakapokuwa ukienda au kutoka maliwatoni. 

Hakikisha vyombo vinavyotumika kuandaa chakula cha mtoto vimeoshwa vizuri kwa maji safi na sabuni. Iwapo una msaidizi wa kazi msisitize mara kwa mara kuzingatia usafi wa vyombo ikiwemo mbinu za ukaushaji wake na maeneo anayohifadhi. 

Kuna baadhi wanaandaa chakula na kukaa muda mrefu bila kumlisha mtoto, hii si sawa. TFNC inashauri kuwa mlishe chakula mtoto baada ya kukitayarisha achana na mambo ya kumlisha viporo au chakula kilichobaki. 

Kwa makala kama haya “subscribe” kwenye jarida letu la kila wiki la Jiko Point. Iwapo unahitaji kufahamu jambo fulani la chakula na nishati kutoka kwa wataalamu tuma meseji au Whatsapp kupitia +255 677 088 088

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa