Fausta Ntara: Mwanamke kinara utengenezaji majiko banifu Kanda ya Ziwa

Na Mariam John
13 Jun 2022
Aliacha ualimu wa shule ya msingi ili kujikita katika kazi hiyo. Anamiliki kampuni ya kutengeneza majiko hayo jijini Mwanza. Majiko hayo yanatumia kuni na mkaa kidogo, hivyo kupunguza ukataji miti. Ni miaka 30 imepita tangu aache kazi ya ualimu kwa kile alichodai ni maslai duni katika kazi yake.  Aliamua kujiajiri ili kutengeneza fedha zake mwenye […]
article
  • Aliacha ualimu wa shule ya msingi ili kujikita katika kazi hiyo.
  • Anamiliki kampuni ya kutengeneza majiko hayo jijini Mwanza.
  • Majiko hayo yanatumia kuni na mkaa kidogo, hivyo kupunguza ukataji miti.

Ni miaka 30 imepita tangu aache kazi ya ualimu kwa kile alichodai ni maslai duni katika kazi yake. 

Aliamua kujiajiri ili kutengeneza fedha zake mwenye kwa kuanzisha shughuli za ujasiriamali katika sekta ya nishati ya kupikia. 

Fausta Ntara (66) ni Mkurugenzi wa kampuni ya Jiko Bora iliyopo mkoani Mwanza inayojishughulisha na kutengeneza majiko banifu yanayotumia kuni na mkaa kidogo.

Fausta anaendesha kampuni hiyo ambayo shughuli zake zinazochangia kupunguza ukataji wa miti kwa usaidizi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido). 

Safari ya ujasiriamali ya mama huyo mwenye watoto wa tatu haikuwa rahisi kwa sababu baada ya kuacha kazi ya ualimu alianza kufanya biashara ya kuuza mbao kabla ya kugeukia utengenezaji majiko banifu. 

Hata hivyo, wenzake alioanza nao kazi hiyo hawakudumu naye muda mrefu kwenye kikundi chao. Walisambaratika baada ya matarajio yao kutofikiwa.

“Tulianza kama kikundi cha wajasirimali kama 10 hivi baadaye wenzangu kila mmoja kwa wakati wake aliacha akiamini kazi hiyo ni ngumu kutokana na kucheza na udongo kila siku unachafua nguo na hata kucha,” anasema Fausta. 

Mama huyo ambaye amewahi kufundisha katika Shule ya Msingi Nyakato anasema licha ya kukimbiwa na wenzake hakukata tamaa ya kutimiza ndoto zake kuanzisha kampuni ya kutengeneza majiko banifu. 

Lengo lilikuwa ni moja tu kuungana na wadau kutunza mazingira na kufungua milango ya ajira kwa vijana na wanawake.

“Mimi ni mwanamazingira nikaona kuendelea kuharibu mazingira kwa kuuza mbao si sahihi nikaona bora nitafute mbinu mbadala itakayosaidia katika kutunza mazingira japo kwa kiasi fulani ndipo nikaanza kutengeneza majiko banifu,” anasema Fausta.

Mjasiriamali anayejishughulisha na utengenezaji wa majiko banifu, Fautsa Ntara akimwonyesha mteja majiko anayotengeneza ambayo hutumia kuni na mkaa kidogo kupikia chakula. Picha | Mariam John.

Pamoja na kuanzisha kampuni ya kutengeneza majiko banifu, Fausta anakiri kuwa safari ya utunzaji wa mazingira bado ni ndefu ikizingatiwa kuwa ukataji wa miti ni mkubwa kuliko uhifadhi.

Mipango yake ya baadaye ni kuanza kutengeneza mkaa mbadala unaotokana na vumbi la mbao na takataka ili kutafuta suluhu endelevu zitakazosaidia kuokoa miti. 

“Ni matarajio yangu ya baadaye iwapo nitapata mashine nitaanza kutengeneza mkaa mbadala ambapo nitakuwa naenda Buhindi ambako wanaranda mbao naenda kuzoa magunia ya vumbi la mbao kisha nakuja kutengeneza mkaa mbadala kwa kuchanganya na unga kidogo wa makaa ya mawe,” anasema Fausta akiendelea na shughuli zake katika ofisi yake iliyopo Sido Mkoa wa Mwanza.

“Majiko banifu ni ajira”

Fausta anasema kazi ya kutengeneza majiko banifu siyo “ya kitoto” kwa sababu inahitaji nguvu na muda kuikamilisha.

Pamoja na ugumu wa kuyatengeneza kajiko hayo, anajivunia kazi hiyo kwa sababu imemfanya kuwa sehemu ya kutunza mazingira na kutoa ajira.

Kampuni yake imefanikiwa kuajiri watu watano wanaomsaidia katika kazi za kila siku ikiwemo kutafuta udongo wa mfinyanzi na waundaji wa majiko hayo kwa aina tofauti.

Kazi ya kutengeneza majiko banifu inamsaidia kupata fedha za kujikimu kimaisha na kumpunguzia utegemezi kwa watoto wake ambao amewasomesha kutokana na mapato ya kazi hiyo.

Aina ya majiko anayotengeneza

Fausta anatengeneza majiko ya aina tatu: Jiko Smart linalotumia mkaa na kuni, Jiko Matawi linalotumia mkaa peke yake; na Jiko la Kawaida ambalo ni dogo maalumu kwa kuni na mkaa.

Majiko haya hutumia mkaa au kuni kidogo na kuivisha chakula kigumu ikiwemo maharage, makande ama chakula chochote ambacho hukaa jikoni muda mrefu na kupunguza matumizi ya kuni nyingi.

“Yanafaa pia kwa watu wanaoishi kijijini badala ya mama kufunga mzigo wa kuni kila siku kwenda nao nyumbani anapotoka shambani, majiko haya yanamasaidia mzigo mmoja kutumia kwa wiki moja na zaidi,” anasisitiza Fausta.

Baadhi ya majiko anayotengeneza Fausta yanayotumia kuni na mkaa kidogo ili kupunguza ukataji wa miti. Picha | Mariam John.

Namna yanavyotengenezwa

Ili kuunda jiko hilo, vitu vinne hadi vitano vya msingi vinahitajika ambavyo ni udongo, majivu, bati, nondo na saruji.

Wakati wa kuanza kuunda jiko hilo, udongo huuchanganywa na majivu kisha kulowekwa kwa muda wa siku tatu ili kuondoa gesi.

“Udongo unapokuwa na gesi husababisha jiko kuharabika haraka,” anasema Fausta na kueleza kuwa hatua inayofuata ni kufyatua jiko kwa muundo unaoutaka na kuliacha kivulini kwa muda wa siku tano kabla hatua nyingine inayofuata. 

Muundo wa juu wa jiko huandaliwa kwa kukunja bati na kisha kupakwa udongo wa saruji ambao husaidia muundo wa ndani ya jiko usibanduke. Baada ya hapo jiko huwa tayari kwa ajili ya kupelekwa sokoni.

Majiko hayo huuzwa kwa wananchi wa kawaida kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, mama lishe na taasisi zinazotumia kwa matumizi makubwa zikiwemo shule. 

Jiko moja huuzwa kati ya Sh15,000 hadi Sh100,000 kutegemeana na ukubwa na aina ya jiko husika. Pia mjasiriamali huyo hutengeneza majiko banifu maalum kwa uokaji wa mikate na keki.

Hata hivyo, Fausta anasema akiimarika zaidi kibiashara  anatarajia kuboresha teknolojia ya kutengeneza majiko banifu ili kuongeza uzalishaji na soko la bidhaa hizo.

Anavyowapata wateja wake

Mara nyingi hutangaza biashara yake kupitia kwa wateja wanaokuja kununua majiko lakini pia kupitia kwenye maonyesho ya wafanyabiashara kama Nane Nane na maonyesho ya wafanyabiashara wadogo.

“Siwezi kutangaza biashara yangu mitandaoni…, ila ninapata wateja kutoka kwa wateja wangu wanaonunua majiko hapa, kwa siku naweza kuuza jiko tatu hadi nne,” amesema Fausta.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa