Hilda avunja tena rekodi ya Guinness, apika tani 8 za Jollof kwa saa 8

Na Lucy Samson
16 Sept 2025
Mpishi maarufu wa Nigeria Hilda Baci, ameandika historia mpya baada ya kuvunja tena rekodi ya Guinness kwa kupika zaidi ya tani nane  za wali wa jollof kwa muda wa saa nane
article

Zaidi ya sahani 16,000 za wali wa Jollof uliopikwa zilisambazwa kwa wananchi.


Mpishi maarufu wa Nigeria Hilda Baci, ameandika historia mpya baada ya kuvunja tena rekodi ya Guinness kwa kupika zaidi ya tani nane  za wali wa jollof kwa muda wa saa nane, tukio lililompatia heshima ya dunia na kuibua shangwe miongoni mwa mashabiki wa mapishi Afrika.

Jaribio hilo lililofanyika Victoria Island, Lagos, Septemba 12, 2025  liliwakutanisha mamia ya mashabiki na wapenda chakula, huku wataalam wa rekodi ya dunia ya Guinness wakihesabu na kuthibitisha uzito halisi wa wali uliopikwa.

Hilda (29) ambaye jina lake halisi ni Hilda Bassey, amenukuliwa akisema kuwa kazi hiyo haikuwa rahisi lakini ameridhika na kufurahishwa baada ya kuweka rekodi hiyo kwa mara nyingine tena.

“Sikutegemea itakuwa ngumu kiasi hiki na imekuwa changamoto kweli. Ni kazi kubwa sana lakini inaridhisha mno kufanikisha rekodi hii.

…Ushindi  huu pia ni mali ya wananchi wa Nigeria kwa kuwa wote wamechangia katika mafanikio haya.” amesema Hilda.

Kutokana na ukubwa wa sufuria hiyo, timu ya wapishi wa Hilda ilihitaji usaidizi wa ziada kufunika na kufunua mfuniko ilipohitajika.Picha/Reuters.

Chakula  alichokipika Hilda kilihusisha zaidi ya kilo 4,000 za mchele wa basmati uliooshwa (takriban asilimia ya uzito wote), kilo 164 za nyama ya mbuzi, kilo 220 za ‘cubes’ (kiungo cha kupikia) za Gino Asun na kuku wa pilipili pamoja na kilo 600 za mchanganyiko wake maalum wa pilipili za jollof.

Msosi huo ulipikwa katika sufuria kubwa yenye uwezo wa kubeba lita 23,000 zinazoweza kulinganishwa na tenki dogo la maji au kwa upana ikafananishwa na meza kubwa ya duara ya ofisini inayoweza kukaliwa na watu 10 mpaka 12.

Kwa mujibu wa Hilda zaidi ya sahani 16,000 zilisambazwa kwa wanachi waliokuwa wamekusanyika katika maeneo hayo kushuhudia rekodi hiyo kama ilivyoainishwa katika masharti ya Guiness ya kukitaka chakula hicho kutokutupwa.

Hii si mara ya kwanza kwa Hilda kuvunja rekodi ya dunia katika upande wa mapishi, Mei  2023  mwanadada huyo alivunja rekodi kwa kupika vyakula mbalimbali kwa muda wa saa 93 na dakika 11 mfululizo, rekodi ambayo haijawahi kuvunjwa mpaka sasa.

Hilda alishirikiana na wapishi wengine zaidi ya sita waliofanikisha kuweka rekodi hiyo mpya ya mapishi duniani.Picha/REUTERS.

Rekodi hiyo iliyovutia umakini wa dunia na hata kuielemea tovuti ya Guinness World Records kutokana na wingi wa watu waliotaka kufuatilia huku ikitoa motosha kwa waafrika kutengeneza rekodi zao wenyewe.

Ushindi wa Hilda pia ni ishara ya kuendeleza “Vita vya Jollof” ubishani wa muda mrefu kati ya Nigeria na Ghana kuhusu nani hupika jollof bora zaidi.

Hadi sasa, rekodi ya jollof ya mtindo wa Ghana haina mmiliki, jambo linalotoa nafasi kwa wapishi wa Ghana kutengeneza rekodi yao.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa