Kampeni ya ‘Mamalishe na Samia kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia Tanzania

Na Lucy Samson
13 Feb 2025
Mwanamuziki na mama lishe maarufu nchini Zuwena Mohamed (Shilole) amezindua kampeni ya ‘Mamalishe na Samia’ yenye lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi kwa wafanyabiashara wanaojishughulisha na kuuza chakula nchini.
article
  • Itaanza kufanyika katika wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam na baadae kuifikia nchi nzima.

Mwanamuziki na mama lishe maarufu nchini Zuwena Mohamed (Shilole) amezindua kampeni ya ‘Mamalishe na Samia’ yenye lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi kwa wafanyabiashara wanaojishughulisha na kuuza chakula nchini.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Februari 13, 2025 Shilole amesema kampeni hiyo inalenga kuwapongeza Mama Lishe nchini pamoja na kuwasaidia kwa kuwapa vifaa vya kupikia ambavyo vinatumia nishati safi.

“Mama lishe imekuja kukomboa mama lishe tumtoe kwenye kupikia kuni na mkaa aende kwenye kutumia nishati safi ya kupikia…kila mtanzania anatakiwa kutumia jiko la gesi, umeme pamoja na nishati mbadala,” amesema Shilole.

Kampeni hiyo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia kuhamasisha matumizi ya  nishati safi ya kupikia ili kufikia asilimia 80 ya watumiaji wa nishati hiyo sawa na iliyoainishwa na Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa mwaka 2024.

Ili kufikia lengo hilo, Serikali pamoja na wadau mbalimbali wameendelea kutoa elimu na kusambaza majiko ya nishati safi ikiwemo gesi atika maeneo mbalimbali nchini ili watu wengi zaidi wahamasike kutumia nishati hiyo.

Januari 27 mwaka huu wasanii wa maagizo kutoka Kundi la Lamata na Warembo wa Samia Queens wametoa Mitungi ya gesi 300 kwa Mama Lishe na Baba Lishe katika soko la samaki la feri, lilipo ilala jijini Dar es Salaam lengo ikiwa ni kuongeza watumiaji wa nishati hiyo nchini.

Aidha Shilole amesema kampeni hiyo inatarajiwa kwenda nchi nzima lakini kwa sasa itafanyika katika wilaya za Mkoa Wa Dar es Salaam huku ratiba ya mikoa mingine ikitarajiwa kutolewa siku chache zijazo.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa