Nyama, mayai na maziwa vimeelezwa katika ripoti mpya ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kuwa ni chanzo muhimu cha virutubisho vinavyohitajika mwilini ambavyo haviwezi kupatikana kwa urahisi katika lishe itokanayo na mimea.
Ripoti hiyo ya “Mchango wa chakula cha asili cha wanyama wa nchi kavu kwa lishe bora na matokeo yenye afya” inaeleza kuwa katika hatua za awali za maisha kama ya ujauzito na unyonyeshaji, utoto, umri wa balehe na uzeeni virutubisho vya vyakula hivyo vinahitajika sana.
Hii ni tathimini ya kwanza ya kina ya FAO iliyoangalia faida na hasara za kula vyakula vitokanavyo na wanyama na inatokana na ushahidi kutoka kwa nyaraka zaidi ya 500 za kisayansi na sera 250.
FAO inasema sahani ya nyama ya kusindikwa , mayai na glasi ya maziwa pembeni vinaweza kukupa virutubisho vya msingi kama protini, mafuta na wanga na pia virutubisho vingine ambavyo ni vigumu kupatikana kutoka kwenye mimea kwa ajili ya kiwango na ubora wa lishe inayohitajika mwilini.
Protini yenye ubora wa juu, idadi ya asidi muhimu ya mafuta pamoja na madini ya chuma, ‘calcium, zinc, selenium, Vitamini B12, choline’ na madini mengine kama vile (carnitine, creatine, taurine) hutolewa na vyakula kutoka shambani na wanyama wengine wafugwao vina umuhimu na kufanya kazi kubwa za afya na maendeleo ya kimwili.
FAO imebainisha kuwa madini ya chuma na vitamini A ni kati ya upungufu wa kawaida wa virutubisho kote ulimwenguni, haswa kwa watoto na wanawake wajawazito.
Zaidi ya mtoto mmoja kati ya watoto wawili wa shule ya awali ambao ni takriban watoto milioni 372 na wanawake bilioni 1.2 walio katika umri wa kuzaa, kulingana na utafiti uliochapishwa katika gazeti la Lancet, wanakabiliwa na ukosefu wa angalau moja ya virutubishi vidogo vitatu ambavyo ni madini ya chuma, vitamini A au zinki.
Robo tatu ya watoto hawa wanaishi Kusini na Mashariki mwa Asia, Pasifiki na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kuku ni mali inayoshikiliwa sana kiuchumi na lishe katika jamii za Afrika na mara nyingi husimamiwa na wanawake. Picha | FAO/Believe Nyakudjara.
Kulingana na ripoti hiyo ya FAO, ulaji wa chakula cha wanyama kutoka kwa wanyama hutofautiana sana ulimwenguni kote.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa mfano, mtu hutumia wastani wa gramu 160 tu za maziwa kwa mwaka, wakati mkazi wa maisha ya wastani wa Montenegro, hutumia kilo 338.
Ukiangalia katika suala la mayai, mtu wa Sudan Kusini hutumia gramu 2 kwa wastani kwa mwaka ikilinganishwa na wastani wa kilo 25 kwa mtu wa Hong Kong.
“Mtu wa kawaida nchini Burundi hutumia kilo 3 tu za nyama kwa mwaka, ikilinganishwa na kilo 136 zinazoliwa kwa mtu anayeishi Hong Kong,” limesema shirika la FAO.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaweka wazi kuwa “ulaji wa hata kiwango kidogo cha nyama nyekundu iliyochakatwa inaweza kuongeza hatari ya vifo na matokeo ya magonjwa sugu, ikiwa ni pamoja na magonjwa ya moyo na mishipa na saratani ya utumbo mpana.”
Ulaji wa nyama nyekundu ambayo haijasindikwa kwa kiasi cha wastani huenda ukawa na hatari ndogo.
Wakati huo huo FAO inasema ushahidi kuhusu uhusiano wowote kati ya maziwa, mayai na ulaji wa kuku kwa watu wazima wenye afya nzuri na magonjwa kama vile ugonjwa wa moyo, kiharusi na shinikizo la damu haujathibitishwa kwa maziwa au sio muhimu kwa mayai na kuku.