Huenda matumizi ya nishati ya kuni na mkaa yakapungua nchini baada ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kuanza kufundisha wajasiriamali kutengeneza majiko banifu yanayotumia mkaa na kuni kidogo.
Meneja wa Sido Mkoa wa Mwanza, Bakari Songwe amesema hadi sasa vipo viwanda viwili vinavyotengeneza majiko banifu yatakayosaidia kupunguza uharibifu wa mazingira lakini pia kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa.
Viwanda hivyo kuwa ni Victoria Engineering pamoja na Jiko Bora vilivyopo mkoani hapa na kuwa wanazalisha majiko ya aina tofauti yakiwemo yanayotumia nishati ya jua na mengine yanayotumia mkaa kidogo.
“Utengenezaji wa majiko banifu ni moja ya ajenda zetu ambapo ni uendelezaji wa masuala ya ukuaji wa teknolojia pamoja na kupunguza uharibifu wa mazingira,” amesema Songwe.
Kinachofanyika hivi sasa ni kutangaza majiko hayo kwenye mitandao ya kijamii na tovuti ya shirika ili wananchi waweze kufahamu uwepo wa bidhaa hiyo na kutoa elimu ya utengenezaji na matumizi ya majiko hayo ili kuisaidia jamii katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.
“Si kwenye mitandao ya kijamii tu pia tunatangaza bidhaa hizo kupitia maonyesho mbalimbali mathalani maonyesho ya Sido Taifa, Sido kanda ya Ziwa, maonyesho ya wajasiriamali wadogo wa Afrika Mashariki maarufu kwa jina la Jua Kali, Nane Nane.
“Kupitia maonyesho hayo watu hupata wasaa wa kuona bidhaa zinazozalishwa na Sido yakiwemo majiko banifu,” amesema Songwe.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Taifa ya Takwimu za Mazingira ya mwaka 2017 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha ukataji miti kinakadiriwa kuwa ni hekta 372,000 kwa mwaka.
Kutokana na changamoto hizo za ukataji wa miti ambazo zinachangia mabadiliko ya tabianchi, baadhi ya wadau wa mazingira wanaendelea na jitihada za kutafuta suluhu endelevu za kupunguza tatizo hilo nchini Tanzania.
Safari bado ndefu matumizi ya nishati mbadala kwa wajasiriamali
Jiko Point imetembelea katika soko la Samaki Kamanga jiji Mwanza, shughuli kuu inayofanyika kwa wajasiriamali hawa ni kuuza na kununua dagaa na samaki waliokaangwa.
Nishati kuu inayotumika katika maandalizi ya samaki na dagaa hao ni kuni, wenyewe wanasema zinarahisisha katika ukaangaji kutokana na makalai yanayotumika kuwa makubwa.
Wakizungumza na Nukta Habari wachuuzi hao wanasema angalau sasa Sido wamekuja na njia ya kupunguza matumizi makubwa ya nishati ya kuni kwa ajili ya kupikia lakini swali lao linabaki kuwa majiko hayo yataweza kuhimili makalaai yao ya kukaangia?
Anjelina Soteli, muuza dagaa waliokaagwa ndani na nje ya Mwanza anasema matumizi ya kuni kwenye eneo hilo ni makubwa kwani kwa kila mchuuzi kiwango cha chini anachotumia kukaangia dagaa si chini ya Sh5,000 na kuwa kiwango hiki kinategemeana na kiwango cha dagaa alichonacho mchuuzi kwa siku hiyo.
Hata hivyo, amesema majiko ya Sido yatawasaidia kupunguza matumizi ya kuni na hivyo kuwa sehemu ya kutunza mazingira huku akiomba watengenezewe yanayokidhi mahitaji yao.
Mfanyabiashara mwingine, Happy Maro anasema matumizi ya majiko hayo yatapunguza matatizo ya kiafya yanayosababishwa na moto mkali pamoja na moshi.
“Kwanza kwa sasa afya zetu ziko hatarini kwakuwa kila siku tunakaa kwenye moto mkali na moshi, ni kweli tunatafuta hela lakini kiafya inatuathiri sana,” amesema Happy
Happy anashauri serikali ipunguze gharama za matumizi ya gesi ili isaidie kwenye shughuli zao hizo.
“Kwa sasa matumizi ya gesi yapo juu, nyumbani kwenye tunaziogopa sanjari na kutumika kukaangia samaki itatugharimu sana,” amesema Happy.
Mwenyekiti wa soko hilo, Mathayo Nyanda ameishauri Serikali kuangalia namna ya kupunguza gharama kujaza mitungi ya gesi ili isaidiei katika matumizi ya kila siku na kwamba itasaidia katika kutunza mazingira.
“Tunalazimika kutumia kuni kwakuwa gharama za maisha zipo juu, kila kitu hakishikiki si kwenye gesi au vitu vingine hivyo mjasiriamali anaona kuliko kujaza gesi mtungi mkubwa kwa gharama ya Sh54,000 na utumike siku nne au tano ni bora nunue kuni za Sh5,000 ili kukaangia dagaa wake,” amesema Nyanda.
Mwenyekiti huyo pia anasema changamoto nyingine ni kuhusu vifaa wanavyotumika katika kukaanga dagaa hao kuwa wanatumia makalai makubwa ambayo hayawezi kuenea kwenye majiko haya ya kisasa.
“Tunaomba sido wabuni majiko makubwa ambayo yataweza kutosheleza makalai haya na kwamba yatasaidia ujasiriamali katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira,” amesema Nyanda.