Matumizi ya umeme kupikia kufanyiwa utafiti wa kina Tanzania

Na Esau Ng'umbi
15 Nov 2022
Lengo ni kuelewa changamoto za matumizi ya nishati ya umeme katika shughuli za upishi na fursa zake.
article
  • Utafanywa kwa ushirikiano na wadau wa nishati kutoka Tanzania, Ujerumani, Bangladesh na Kambodia.
  • Huenda ukasaidia urahisi wa upatikanaji wa nishati ya kupikia 

Dar es Salaam. Wakati mjadala wa kusaka njia bora ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia duniani ukiendelea, nchini Tanzania baadhi ya wadau wa nishati safi wameanza kufanya utafiti utakaotoa suluhu ya kuongeza matumizi ya umeme wakati wa kupika. 

Shirika lisilo la kiserikali la Elico Foundation ambalo ni miongoni mwa watafiti limeeleza kuwa miongoni mwa masuala ambayo utafiti huo utaangazia ni kubaini fursa na changamoto zilizopo kwenye matumizi ya umeme kupikia. 

Utafiti huo wa miezi minne unafanywa na Elico Foundation kwa kushirkiana na wadau wengine wa nishati safi kutoka mataifa ya Ujerumani, Bangladesh,Tanzania pamoja na Kambodia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Elico Foundation, Sisty Basil amesema madhumuni makubwa ya utafiti huo ni kuelewa changamoto za matumizi ya nishati ya umeme katika shughuli za upishi zilizopo hivi sasa pamoja na fursa zinazoweza kupatikana kupitia changamoto hizo.

“Tunataka kuja na majibu ya kina kuhusu vifaa vya kupikia vinavyoweza kukidhi mahitaji yote ya kaya, matokeo ya utafiti huu  yanaweza kutumika katika utungaji wa sera au wakati wa usambazaji wa vifaa hivyo,” amesema Basil katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Hatua hiyo huenda ikachochea upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ambayo itapunguza athari za kimazingira, kiuchumi na kiafya  zinazoendelea kutokea kutokana na kukithiri kwa matumizi ya nishati ya mkaa na kuni.

Hivi karibuni Waziri wa Nishati, January Makamba alieleza kuwa takribani Watanzania 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kupikia mazingira yenye moshi wenye sumu unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni.

Katika utafiti huo, Elico watahusika katika ukusanyaji wa takwimu, ununuzi na usambazaji wa vifaa vya kupikia, kutoa mafunzo kwa wanufaika pamoja na kusimamia dodoso la utafiti kwa kufuata mwongozo wa kimataifa.

Serikali ya Tanzania miaka ya hivi karibuni imekuwa ikihamasisha Watanzania kutumia nishati safi za kupikia kama gesi, umeme na bayogesi ili kuokoa uharibifu wa mazingira na kutunza afya watu. 

Hadi sasa takwimu za wizara ya nishati zinabanisha kuwa ni kaya tano tu kati ya 100 Tanzania zinatumia nishati safi kupikia hususan gesi. 

Katika mkutano wa 27 wa Umoja wa mataifa kuhusu tabianchi (COP 27) Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwaambia washiriki kuwa serikali yake inatarajia kuongeza matumizi ya nishati safi “kutoka asilimia 50 zilizopo hivi sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.” 

Katika utafiti huo wa nishati safi ya kupikia unaofanywa na Elico, wengine ni Programu ya Huduma za kisasa za Nishati ya kupikia (MECS),Taasisi ya Microenergy International (MEI) kutoka nchini Ujerumani, Kampuni ya ME SOLshare Ltd (Solshare) ya nchini Bangladesh pamoja na taasisi ya  ACCESS Advisory.

Kuanza kwa utafiti huo kutasaidia upatikanaji wa takwimu muhimu zitakazosaidia Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wengine kufahamu kwa kina mbinu bora zitakazosaidia kuongeza matumizi ya umemem kupikia. 

Mwanzoni mwa Novemba mwaka huu Makamba aliwataka wadau kufanya zaidi utafiti juu ya athari zitokanazo na matumizi ya nishati ya mkaa na kuni katika kupikia.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa