Dar es Salaam. Ikiwa wewe ni mfuatiliaji wa masuala ya mapishi basi jina la Hilda Baci haliwezi kuwa geni masikioni mwako.
Ni mpishi, mmiliki wa mgahawa na pia mwigizaji, ambaye jina lake halisi ni Hilda Effiong Bassey.
Hilda alizaliwa Septemba 20, 1995, katika Jimbo la Akwa Ibom, nchini Nigeria.
Kabla ya kujulikana kimataifa kupitia mapishi, alihitimu shahada ya Sosholojia katika Chuo Kikuu cha Madonna kilichopo Okija, Jimbo la Anambra nchini Nigeria.
Mbali na taaluma yake ya mapishi, Hilda amewahi kuwa mtangazaji wa kipindi cha televisheni ‘Dine on a Budget’ kinachorushwa kupitia televisheni ya Pop central.
Baci ambaye ndiye mmiliki wa My food by Hilda, biashara ya mgahawa na upishi iliyoko Lagos aliwahi kuigiza kwenye filamu mbalimbali ikiwemo ‘A Walk on Water’ ya mwaka 2021, ‘Mr & Mrs Robert’ 2023 na ‘Everybody Loves Jenifa’ ya mwaka 2024.
Mwanadada huyu ni miongoni mwa wapishi wachache wanaoliwakilisha vyema bara la Afrika katika rekodi za dunia katika tasnia ya mapishi.
Baci ambaye ametimiza miaka 30 leo alianza kugonga vichwa vya habari vya dunia mwaka 2023 alipovunja rekodi ya Dunia (Guiness World Record) ya kupika vyakula mbalimbali kwa muda wa saa 93 na dakika 11 mfululizo.
Rekodi hiyo iliyovutia umakini wa dunia na hata kuielemea tovuti ya Guinness World Records kutokana na wingi wa watu waliotaka kufuatilia huku ikitoa motisha kwa waafrika kutengeneza rekodi zao wenyewe.
Kabla ya Hilda, rekodi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Lata Tondon kutoka India, aliyepika kwa muda wa saa 87 na dakika 45 mwaka 2019.
Hata hivyo rekodi ya Hilda ilivunjwa miezi sita tu baadae na
Alan Fisher, mpishi kutoka Ireland, aliyepika kwa muda wa saa 119 na dakika 57 Novemba 2023.
Baada ya hapo, Evette Quoibia, mpishi mwenye asili ya Liberia na Australia, alivunja rekodi za wapishi hao wawili Februari 2024 baada ya kupika kwa muda wa saa 140, dakika 11 na sekunde 11, na kuweka alama mpya ya kihistoria.
Sasa mwaka 2025 Hilda alifanya jaribio lingine la kuweka rekodi ya dunia kwa kupika Jollof rice chakula kilichoweza kulisha zaidi ya watu 16,600.
Mapishi hayo yalihusisha takribani kilo 4,000 za mchele wa basmati uliosafishwa, kilo 612 za mafuta ya kupikia, kilo 800 za kuku wa Gino Asun peppered chicken pamoja na party jollof, kilo 600 za mchanganyiko maalum wa pilipili za Jollof.
Vile vile, kilo 220 za Gino Asun & peppered chicken cubes, gramu 20 za kiungo cha curry cha Gino pamoja na gramu 7 za thyme ya Gino, kilo 300 za mchanganyiko wa vitunguu maji, kitunguu saumu na tangawizi, kilo 164 za nyama mbichi ya mbuzi, na kilo 1,200 za gesi kwa ajili ya kupikia.
Chakula kilipikwa kwenye sufuria kubwa yenye uwezo wa kubeba lita 23,000, ukubwa unaoweza kulinganishwa na tenki dogo la maji au meza ya duara ya ofisini inayoweza kukaliwa na watu 10 mpaka 12.
Baada ya kupika kwa saa tisa, zoezi hilo lilikaribia kuharibika baada ya chungu kikuu kupasuka wakati wa kupimwa uzito, lakini kwa msaada wa waliokuwepo, hakuna mchele uliomwagika.
Hatimaye wali huo uliweza kulisha zaidi ya watu 16,600 waliokuwepo eneo la tukio.
Wali wa Jollof ni chakula maarufu Afrika Magharibi, ukipikwa kwa mchuzi wa nyanya na mara nyingi kuliwa na nyama au samaki wa baharini, huku ukiwa ni mlo unaounganisha jamii nyingi za eneo hilo.
Mbali na rekodi na majaribio yake, Baci pia amejitolea kufundisha wengine kupitia madarasa ya mapishi mtandaoni, akiwahamasisha wapishi chipukizi.
Ingawa jaribio lake la wali wa Jollof bado halijathibitishwa rasmi na Guinness World Records, limebaki kuwa tukio la kihistoria si tu kwa Nigeria, bali kwa bara zima la Afrika.
Makala hii imeandikwa na Lucy Samson, Fatuma Hussein imehaririwa na Esau Ngu’mbi.