Miradi ya jotoardhi yashika kasi Mbeya, Songwe

Na Daniel Samson
22 Sept 2022
Matumizi ya nishati jadidifu yanazidi kushika kasi Tanzania, baada ya kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Nchini (TGDC) kujipanga kuzalisha umeme wa megawati 200 unaotokana na jotoardhi ifikapo mwaka 2025.
article
  • Inaendeshwa na kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC).
  • Bodi mpya ya TGDC yaridhishwa na utekelezaji wake.
  • Kuzalisha megawati 200 ifikapo 2025.

Matumizi ya nishati jadidifu yanazidi kushika kasi Tanzania, baada ya kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Nchini (TGDC) kujipanga kuzalisha umeme wa megawati 200 unaotokana na jotoardhi ifikapo mwaka 2025.

Kwa mujibu wa TGDC, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha umeme wa jotoardhi usiopungua megawati 5,000 katika maeneo zaidi ya 50 katika mikoa 16 nchini. 

Ili kufikia lengo la kuzalisha umeme wa jotoardhi wa megawati 200, TGDC inatekeleza miradi mitano ya kipaumbele ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. 

Miradi hiyo ni Ngozi megawati 70 na Kiejo-Mbaka (megawati 60) iliyopo Mbeya, Songwe (megawati 5) mkoani Songwe, Luhoi (megawati 5) Pwani, na Natron megawati 60 mkoani Arusha.

Bodi ya TGDC yaridhishwa na kazi

Licha ya TGDC kuendelea na miradi yake mitano ya jotoardhi, imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu kuhakikisha inatekelezwa kama ilivyopangwa ili kuwanufaisha Watanzania na Taifa hasa kuwapatia nishati endelevu na rafiki kwa mazingira. 

Bodi ya TGDC imefanya ziara ya siku tatu kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na kampuni hiyo mikoani Mbeya na Songwe akiambatana na uongozi wa kampuni hiyo ili kujionea utekelezaji wake.

Ziara hiyo ambayo ni ya kwanza tangu bodi hiyo ilipozinduliwa Julai 2022,  iliongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Shubi Kaijage ambaye ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo ya TGDC, kampuni tanzu hii ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

“Tumefarijika na maendeleo na jitihada zinazoendelea katika miradi ya jotoardhi, na tunaendelea kuishauri na kuielekeza Menejimenti ya TGDC ili tufikie malengo ya megawati 200 ifikapo mwaka 2025 kama mipango mikakati ya kampuni ilivyoainishwa  na kutimiza malengo ya Serikali yetu,” amesema Prof Kaijage. 

Nishati ya jotoardhi ina matumizi mengi ikiwemo kuzalisha umeme ambao hutumika kuendeshea mitambo, kupikia na kutoa mwanga majumbani.

Kwa mujibu Kaimu Meneja Mkuu wa TGDC Mhandisi Shakiru Idrissa, kazi ya kuchoronga visima vya jotoardhi itafanyika kwa kipindi cha miezi minne hadi sita kwa upande wa mradi wa Ngozi baada ya kuwasili kwa mtambo mwishoni mwa Oktoba. 

“Kampuni inategemea kupata Megawati 70 za awali kwa vipindi vya awamu mbili, awamu ya kwanza megati 30 na ya pili megawati 40 ifikapo mwaka 2025 (kwa mradi wa Ngozi),” amesema Mhandisi Idrissa.

Katika ziara hiyo Bodi ya Wakurugenzi ya TGDC ilifika katika mradi wa Kiejo-Mbaka uliopo Mbeya, ambapo TGDC imeishachoronga visima vifupi vitatu vya utafiti ambapo megawati 60 zinatarajiwa kuzalishwa.

Katika mradi wa Songwe, umeme wa jotoardhi wa megawati 5 hadi 38 unaratajiwa kuzalishwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa