Nafasi ya wanawake wenye ushawishi upatikanaji wa nishati safi ya kupikia Tanzania

Na Lucy Samson
4 Nov 2022
Wanawake wenye ushawishi nchini wametakiwa kupaza sauti zao kuwakomboa  wanawake wenzao wanaoathirika na matumizi ya nishati chafu za kupikia ikiwemo kuni na mkaa.
article
  • Ni sauti ya wanawake kwenye jamii ambao ni waathirika wa nishati chafu. 
  • Wanaweza kuwasaidia wanawake kujikomboa kiuchumi kupitia nishati safi. 
  • Balozi wa Norway aahidi ushirikiano zaidi kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Dar es Salaam. Wanawake wenye ushawishi nchini wametakiwa kupaza sauti zao kuwakomboa  wanawake wenzao wanaoathirika na matumizi ya nishati chafu za kupikia ikiwemo kuni na mkaa.

Inakadiriwa kuwa watu 33,000 nchini Tanzania wanafariki dunia kila mwaka kutokana na kuvuta sumu za moshi unaotoka kwenye kuni na mkaa wakati wa kupika. 

Mbali na athari za kiafya ambazo zinachangia uwepo wa zaidi ya theluthi mbili ama asilimia 70 za magonjwa ya upumuaji, matumizi ya nishati zisizo safi yanachangia ongezeko la hewa ya ukaa inayochafua mazingira na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Wito huo umetolewa na wanawake wasomi walikuwa sehemu ya jopo lililojadili mada ya mchango wa wanawake wenye ushawishi kuhamasisha matumizi ya nishati safi za kupikia Tanzania.

Walioshiriki kwenye jopo hilo ni wanawake waliowahi kushika nyazifa mbalimbali za uongozi nchini na nje ya nchi akiwemo Anna Tibaijuka aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wengine walioshiriki ni  Zakia Meghji aliyewahi kuwa Waziri wa Kwanza  Fedha na Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Dk Gertrude Mongella aliyeshika nyazifa mbalimbali ikiwemo Spika mstaafu wa Bunge la Afrika.

Akizungumza kwenye mjadala huo uliofanyika Novemba 1 na 2, 2022 jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Mongella amesema matumizi ya nishati safi yatamkomboa mwanamke ambaye ndiye mtumiaji mkubwa na nishati zisizo safi.

“Lazima tuwakomboe wanawake wa Tanzania kutoka kwenye moshi, kusomba maji na kukata kuni ili apate muda wa kufanya mambo mengine ya maendeleo,” amesema Mongella aliyekuwa mzungumzaji wa kwanza wa mada hiyo.

Wakati Serikali ikihamaisha jamii kupanda miti na kutunza mazingira ili kurudisha ikolojia ya nchi, Zainabu Barabara (51) ni miongoni mwa watu walio mstari wa mbele kutekeleza sera hiyo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Picha| Mariam John.

Kwenye jamii ya kitanzania mwanamke ndiye mwenye jukumu la kupika, kukusanya kuni kuchota maji, kufanya kazi za nyumbani na kulea familia.

Jambo hili limewaweka nyuma wanawake kwa kuonekana kuwa hawafai kujifunza na kufahamu kuhusu masuala mbalimbali ya kiteknolojia au kuingiza kipato kinachoweza kuendesha familia.

Wanawake hao wenye ushawishi kwa pamoja wamepaza sauti zao kwa kutoa hoja mbalimbali ili kumkomboa mwanamke kutoka kwenye kupika kwa kutumia mkaa na kuni na kugeukia nishati safi kama umemejua.

Kwa kuzingatia umuhimu wa masuala ya nishati safi kwa jamii,  Mongella aliyewahi kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki  ameitaka Serikali kuchukua  jitihada za haraka kunusuru Watanzania wanaoathirika na matumizi ya nishati hizo zenye madhara kwa afya.

Kwa kusisItiza jambo hilo, Mongella amesema huu siyo wakati wa Serikali kuandika sera na kuishia kwenye makaratasi na badala yake hatua za utekelezaji zichukuliwe

“Tutaandika mabuku mangapi wenzetu waliopigania uhuru wangeandika mabuku tungefika hapa? Kwahiyo wakati wa mabuku umekwisha ni kuandika tu mkakati tujue tunaenda wapi,” ameongeza Mongella.

Nishati safi za kupikia zinazishauriwa kwa matumizi ni pamoja na mkaa mbadala, gesi, bayomasi, umeme, pamoja na gesi kimiminika ( LPJ).

Wanawake wenye ushawishi waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini wakiongoza mjadala kuhusu matumizi ya nishati safi za kupikia, kuanzia kushoto ni  Dk Gertrude Mongella, Zakia Meghji, Anna Tibaijuka na muendesha mada Dorice Rwebangira. Picha|Wizara ya Nishati.

Msemaji mwingine kwenye mjadala huo uliowahusu wanawake wenye ushawishi alikuwa Anna Tibaijuka aliyewahi kuwa pia Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat) ambaye amezungumzia ushiriki wa wanaume kwenye harakati za mkomboa mwanamke.

“Ukiboresha maisha ya mwanamke moja kwa moja unaboresha maisha ya mume wake, watoto wake na familia yake kwahiyo tuendeleze juhudi za pamoja,” amesema Tibaijuka.

Sambamba na hilo Tibaijuka ambaye  amewahamasisha wananawake juu ya matumizi ya teknolojia zinazolenga kuboresha maisha ikiwemo matumizi ya nishati safi za kupikia.

“Na maendeleo ya teknolojia yaliyopo sasa hivi kutumia gesi ni uamuzi na wanawake msibweteke na  masuala ya kitchen party (sherehe za kapu) tuweke na hela za kujaza mitungi ya gesi kule tunapokwenda” ameongeza Waziri huyoo mstaafu.

 Katikati ya mjadala huo suala la bei za nishati  safi  za kupikia likaibuliwa na Zakia Meghji aliyewahi kuwa Waziri wa kwanza Fedha nchini na Waziri mstaafu wa Maliasili na Utalii aliyetaka bei za nishati hizo zizingatie hali za wanawake wasiokuwa na kipato ambao ndio wanunuzi.

“Kwa sasa mwanaume itabidi ahusishwe kutokana na gharama ya nishati hizo hususani kwa wanawake ambao hawana kipato,” amesema Meghji.

Mashirika ya Kimaataifa yahamisishwa kusapoti wanawake

Mama Mongela ameyataka mashirika na taasisi za kimataifa zinazofanya kazi na Tanzania kuunga mkono harakati za kumkomboa mwanamke kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu ikiwemo kuni na mkaa.

“Mashirika ya kimataifa wekeni hili kwenye ajenda zenu kama mtaka kuisadia Tanzania lazima tuwakomboe wanawake wa Tanzania kutoka kwenye moshi, kusomba maji na kukata kuni ili apate muda wa kufanya mambo mengine ya maendeleo,” amesema Mongella.

Naye Balozi wa Norway nchini Tanzania Elizabeth Jacobsen amesema nchi yake inayoshirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo inaweza kuongeza ushirikiano zaidi kwenye masuala ya nishati safi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa