Nishati safi ya kupikia kuwakomboa wanawake kiuchumi Afrika

Na Lucy Samson
14 May 2024
Kwa Mujibu wa Rais Samia watu milioni 900 wanatumia nishati zisizo salama kupikia licha ya athari za kiafya na kimazingira zilizopo.
article

Watu milioni 900 wanatumia nishati zisizo safi kupikia.
Rais Samia aomba wabia wa maendeleo kuchangia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.


Rais Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia katika nchi za Afrika ni miongoni mwa njia zitakazomkomboa mwanamke kiuchumi pamoja na kulinda mazingira yanayoharibiwa na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa nishati safi ya kupikia uliofanyika katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Paris, Ufaransa leo Mei 14, 2024 amesema matumizi ya nishati safi yataongeza ujumuishi wa kijinsia katika shughuli za kiuchumi.

“Upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia utatoa fursa zaidi kwa wanawake kushiriki katika shughuli nyingine za kiuchumi, kukomesha umaskini na kutokuwepo kwa usawa,” amesema Rais Samia.

Nishati safi ya kupikia ni miagoni mwa ajenda zinazojadiliwa sana miaka ya hivi karibuni kutokana na kukithiri kwa athari za mabadiliko ya tabia ya nchi na uharibifu wa mazingira.

Kwa Mujibu wa Rais Samia watu milioni 900 wanatumia nishati zisizo salama kupikia licha ya athari za kiafya na kimazingira zilizopo.

Mei 2024 Serikali ya Tanzania ilizindua Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2024 hadi mwaka 2034.

Lengo la mkakati huo ni kunusuru maisha ya Watanzania pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwemo ukataji miti ambapo hekta 469,000 zinakadiriwa kuteketea kila mwaka nchini.

Wadau, wabia kuongeza matumizi ya nishati safi Afrika

Ili kuondokana na matumizi ya nishati zisizo salama, Rais Samia amewaomba wadau wa maendeleo na wafadhili ikiwemo Benki ya Dunia (WB) kuchangia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia Afrika.

Ameongeza kuwa ili kuongeza matumizi ya nishati hiyo ni vyema viongozi wakatafanya tafiti za kutosha na kushirikisha wadau wa maenndeleo kutoka ndani na nje ya bara la Afrika pamoja na kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo Afrika.
“Tunawashukuru wale ambao tayari wamechangia na tunakaribisha ahadi zaidi za hatua za sera, ushirikiano mzuri, na msaada katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wote,” amesema Rais Samia.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa