Oryx, ubalozi wa China wagawa mitungi 800 kwa walimu, waandishi wa habari, watumishi wa Serikali Arusha

Na Lucy Samson
7 Oct 2024
Mitungi hiyo itasaidia kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa  makundi hayo nchini.
article
  • Mitungi hiyo itasaidia kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa  makundi hayo nchini.

Kampuni ya Oryx kwa kushirikiana na ubalozi wa China nchini Tanzania wamegawa mitungi ya gesi 800 kwa walimu, watumishi wa Serikali na waandishi wa habari jijini Arusha ili kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo nchini.

Mrisho Gambo, Mbunge wa jimbo la Arusha, aliyekuwa Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mitungi hiyo leo Oktoba 7, 2024 amesema mitungi hiyo itasaidia kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa  makundi hayo.

“Ukitaka jambo lako lifike mbali lazima lipitie kwa walimu…wao watatusaidia kwenda kufikisha elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari lakini hata majumbani,” amebainisha Gambo.

Huenda ugawaji wa mitungi hiyo ya gesi ukachagiza kufikia lengo la Serikali kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.

Kampeni hiyo inayopigiwa chapuo na Rais Samia Suluhu Hassan inakuja wakati kukiwa na idadi ndogo ya watanzania wanaotumia nishati hiyo huku matumizi ya kuni na mkaa kupikia yakiendelea kushika kasi kwa silimia 67 kama inavyobainishwa na Ripoti ya Utafii wa Athari za Upatikanaji wa Nishati Endelevu kwa mwaka 2021/2022 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Hiyo ni sawa na kusema zaidi ya nusu au kaya sita kati ya10 zinatumia nishati hiyo kwa ajili ya mapishi huku asilimia 25 wakitumia majiko ya mkaa na asilimia 8.1 majiko mengine.

Baadhi ya majiko ya gesi yalitolewa kwa waandishi wa habari, walimu na watumishi wa Serikali leo katika Hoteli ya Gran Melia Arusha.Picha|Lucy Samson.

Kwa upande wake balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ikiwemo ya nishati safi ya kupikia.

“China itaendelea kusapoti nishati safi ya kupikia na miradi mingine mingi ya maendeleo itakayoendelea Tanzania,” amesema balozi Mingjian.

Ubalozi huo umechangia majiko ya gesi 400 huku 400 mingine yakitolewa na kampuni ya Oryx Tanzania.

Katika hatua nyingine Gambo amebainisha mikakati ya kusambaza nishati safi ya kupikia katika shule zilizopo katika Jiji hilo mradi utakaotumia Sh560 milioni.

Amesema wataanza na shule chache za mfano ambazo zitajengewa mifumo ya nishati safi ya kupikia ili kuhamasisha matumizi ya nishati hizo katika taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kama ilivyoagizwa na Serikali.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa