Rais Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati ya gesi nchini kwa sasa ni suala la lazima kutokana na faida mbalimbali ikiwemo za utunzaji mazingira na afya.
Kiongozi huyo wa nchi aliyekuwa akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba ya mauziano na uendeshaji wa kitalu cha Mnazi Bay amewaambia wahudhuriaji kuwa kutokana na kuogezeka kwa elimu juu ya matumizi ni vyema kwa jamii kuhamia katika matumizi ya nishati hiyo.
“Tulikuwa tunatishana kwamba ukiweka gesi utalipuka nyumba pamoja na wanao…tulipofika hapa hili ni jambo la lazima, sasa majumbani kwetu kwingi tutumie gesi,” amesema Rais Samia Ikulu jijini Dodoma leo Februari 3, 2024.
Aidha, kiongozi huyo amesema kuwa ajenda ya matumizi ya nishati hiyo si ya Tanzania pekee bali ni ya bara zima la Afrika na kwamba atatumia nafasi yake kama kionngozi kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
“Kama mkuu wa nchi nimebaba ajenda hii kwa Afrika kutoa nishati safi na salama kwa wanawake wa Afrika ili wapike kwa nishati safi na salama…
…Suala la kuwa gesi sio anasa kama Serikali tunawajibika kutoa huduma hiyo kwa wananchi kupitia sekta binafsi,” amesema Rais Samia.
Kauli ya Rais Samia ni muendelezo wa harakati za Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo lengo ni kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2030.
Ili kufikia lengo hilo Serikali iliahidi kuweka nguvu kubwa kutoa elimu na uwekeza katika kuwezesha upatikanaji wa nishati safi maeneo ya vijijini ambapo shughuli kubwa za ukataji miti kwa ajili ya mkaa na kuni hufanyika.
Jitihada hizo zitaiokoa Tanzania dhudi ya athari za uharibifu wa mazingira na pia kupambana na athari za mabadiliko yanaendelea nchini na duniani kote.