Serikali ya Tanzania imesema inaendelea na zoezi la utoaji wa ruzuku ya mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) katika maeneo mbalimbali nchini huku ikianisha utaratibu wa wa kununua gesi kwa ruzuku hiyo.
Kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Uliozinduliwa Mei, 2024 Serikali ilibainisha kutoa ruzuku ya asilimia 20 hadi asilimia 50 ya bei ya mitungi ya gesi ili kuchochea matumizi ya nishati hiyo.
Lengo la mkakati huo ni kufikisha asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi hadi itakapofikia mwaka 2034 kutoka asilimia chini ya 10 zilizopo sasa.
Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga aliyekuwa akijibu swali la Kabula Shitobela Mbunge wa Viti Maalum (CCM) aliyetaka kujua utaratibu unaotumika kutoa mitungi hiyo.
“Utaratibu wa sahisahivi kila mtungi mmoja unaenda kwa mtu mmoja na unachukuliwa kwa namba ya NIDA yote ni kuhakikisha tunaweza kufikisha kwa wananchi wengi zaidi,” amesema Kapinga leo Februari 10, 2025 Bungeni Dodoma.
Kapinga ameongeza kuwa utaratibu huo unatumika katika kila mkoa nchi nzima kupitia mawakala maalum walioanishwa na Serikali ambapo kufikia Februari 9, 2025 tayari mitungi 78,500 imeshatolewa kati ya mitungi 445,200 iliyotengwa huku mkoa wa Mwanza ukitengewa mitungi 19,500 kwa bei ya ruzuku.
Aidha Kapinga amebainisha mpango wa kuongeza wakala wa nishati safi ikiwemo gesi na umeme kupitia Wakala wa Umeme vijijini ili kuhakikisha wanachi wengi zaidi wanatumia nishati safi kupikia.